1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Bhutto chapinga kuahirishwa kwa uchaguzi

31 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CiNo

Chama cha Pakistan People´s Party, PPP, cha marehemu Benazir Bhutto, kimepinga vikali hatua ya kuuchelewesha uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika tarehe nane mwezi ujao wa Januari.

Afisa wa serikali ya Paksitan ametangaza kwamba uchaguzi huo utacheleweshwa kwa majuma manne au zaidi kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wa chama cha PPP waziri mkuu wa zamani, Benazir Bhutto.

Afisa huyo wa serikali amesema uchaguzi huo utaahirishwa kwa sababu ya machafuko yanayoendelea nchini Pakistan ambayo yamewaathiri maafisa wa uchaguzi na shughuli za maandalizi ya uchaguzi huo.

Serikali inasema uratibu umetatizwa katika mkoa wa Sindh, nyumbani mwa familia ya Benazir Bhutto na kwamba uchapishaji wa makaratasi ya kupigia kura katika mji mkubwa wa Pakistan, Karachi umechelewa mno.

Ofisi zaidi ya 40 za tume ya uchaguzi na ofisi za utawala zimeharibiwa katika mkoa wa Sindh.

Maafisa wa tume ya uchaguzi nchini Pakistan watakutana kesho kuamua ikiwa waendelee na uchaguzi huo au waucheleweshe kwa muda wa karibu miezi miwili.