1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CDU chaendelea na mkutano wake Kalsruhe

16 Novemba 2010

Kansela Merkel ataendelea kukiongoza chama cha CDU kwa miaka miwili ijayo. Chama hicho kinakabiliwa na changamoto huku majimbo sita kati ya 16 ya Ujerumani yakijiandaa kufanya uchaguzi mwaka ujao

https://p.dw.com/p/QA2b
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: dapd

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa chama cha Christian Democratic Union, CDU hapa Ujerumani, unaendelea kwa siku ya pili na ya mwisho hii leo mjini Kalsruhe. Hapo jana kansela wa Ujerumani Angela Merkel alichaguliwa tena kuendelea kukiongoza chama hicho na asilimia 90 ya wajumbe. Akizungumza kwenye mkutano huo hapo jana Bibi Merkel, aliwahimiza Wajerumani wanaojadili kuwajumuisha waislamu katika jamii, waunge mkono zaidi maadili ya Ukristo, akisema Ujerumani haina tatizo la Uislamu bali uhaba wa Ukristo. Amesema wageni wanaotaka kuishi Ujerumani wanakaribishwa, lakini sharti wajifunze lugha ya Kijerumani na kuheshimu sheria za nchi.

Kansela Merkel pia amewahimiza wanachama wa chama hicho kutotilia maanani kura za maoni zinazoonyesha muungano wake wa mrengo wa kati kulia ukiwa nyuma ya upinzani wa Ujerumani wa mrengo wa kati kushoto.  Amesema Ujerumani inafanya vizuri kuliko nchi nyengine nyingi zilizoathiriwa na mzozo wa kiuchumi.