1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

270311 Berlin Reaktionen Wahlen

28 Machi 2011

Mzozo kuhusu nishati ya nyuklia umechangia kwa kiwango kikubwa matokeo ya chaguzi za majimbo nchini Ujerumani katika jimbo la Baden-Wurttemberg na Rheinland-Pfalz.

https://p.dw.com/p/10iuS
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Kitu kimoja tu ambacho kila mtu alikubaliana nacho baada ya uchaguzi kukamilika jana jioni ni mada muhimu iliyotumiwa kama kigezo na wapigaji kura katika majimbo ya Baden-Wurttenberg na Rheinland- Pfalz; nayo ni sera kuhusu nishati ya nyuklia. Wajumbe wa vyama vyote wamesema janga la nyuklia nchini Japan bila shaka lilitawala mijadala na mitazamo ya wapigaji kura kusini magharibi mwa Ujerumani.

Mageuzi yaliyotangazwa na kansela Angela Merkel, kuhusu kufungwa kwa vinu saba vya nyuklia humu nchini kwa miezi mitatu, hayakutosha kuwashawishi Wajerumani, anasema katibu mkuu wa chama cha Chritian Democratic Union, CDU, Hermann Gröhe:

"Nadhani suala muhimu ni kwamba muda tangu kutokea janga la nyuklia Japan hadi kufikia uchaguzi ulikuwa mchache mno kuweza kuwashawishi wapigaji kura. Kampeni hazipasi kulaumiwa, bali matukio nchini Japan na athari zake kwa sera ya nishati ndio lilikuwa suala walilotumia wapigaji kura kuamua. Hakukuwa na muda kuwashawishi. "

Kansela Merkel ndiye kiongozi pekee wa chama ambaye hakuwa na cha kufurahia jana jioni baada ya uchaguzi kukamilika. Kulikuwa na wingu la wasiwasi na hali ya shinikizo katika jengo la wakfu wa Konrad Adenauer mjini Berlin. Chama cha CDU kilipata pigo huko Baden- Wurttenberg kwa kupata asilimia 39 ya kura, huku kikipoteza pointi tano asilimia ikilinganishwa na uchaguzi uliopita jimboni humo. Waziri mkuu wa sasa wa jimbo la Baden Wuerttemberg, Stefan Mappus, alikiri kushindwa vibaya katika uchaguzi, akiwalaumu wapiga kura kwa kuwa na wasiwasi kuhusu janga la nyuklia katika kiwanda cha Fukushima huko Japan.

Chama cha Kijani chavuma

Landtagswahlen Die Gruenen am 27.03.11
Mwenyekiti wa chama cha kijani, Claudia Roth (kulia)pamoja na viongozi wengine wa chamaPicha: dapd

Hali lakini ilikuwa tofauti kabisa kwa wanachama wa chama cha Kijani. Chama hicho kinajiandaa kumteua waziri mkuu wa kwanza katika historia ya Ujerumani, Winfried Ktretschmann, baada ya kuongeza maradufu idadi ya kura ilizoshinda kufikia asilimia 24. Kiwango hicho kinatosha kukiwezesha chama cha Kijani kuunda serikali ya mseto na chama kikuu cha upinzani cha Social Democratic, SPD, ambacho kimepata asilimia 23 ya kura.

Kulikuwa na shangwe na nderemo katika makao makuu ya chama. Mwenyekiti wa chama hicho, Claudia Roth, alifurahishwa na matokeo ya chaguzi za majimbo huko Baden-Wurttemberg na Rhenland-Pfalz:

"Ni matokeo mazuri na ya kuridhisha kwa chama cha Kijana. Ni siku ambayo mkondo wa siasa za shirikisho la Ujerumani umebadilika kabisa. Bila shaka siku hii na matokeo haya ya uchaguzi ni pigo kubwa kwa sera zitakazosahaulika katika siku zijazo za serikali iliyopo sasa madarakani."

Katika jimbo la Rheinland-Pfalz, wapigaji kura walikiadhibu zaidi chama cha kiliberali cha FDP, kilichomo kwenye serikali ya mseto na chama cha kansela Merkel cha CDU. Chama cha FDP kilipata asilimia 4.2 pekee ya kura na hivyo kushindwa kufikia kiwango kinachostahili kuweza kuwakilishwa katika bunge la mkoa mjini Mainz. Chama cha SPD kilipata asilimia 35.7, hivyo waziri mkuu wa jimbo hilo, Kurt Beck, anatarajiwa kuendelea kushika wadhifa huo katika serikali ya mseto atakayounda na chama cha Kijani ambacho kimeshinda asilimia 15.4 ya kura.

Chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke, hakikufanya vizuri na hakitawakilishwa katika mabunge ya mikoa yote miliwi. Mwenyekiti wa chama hicho, Klaus Ernst amesema hawatavunjwa moyo na matokeo hayo bali wataendelea kutia bidii kuhakikisha wanawakilishwa katika majimbo matatu ambayo hawana uwakilishi mbali na majimbo 13 ambamo wanawakilishwa.

Mwandishi: Marx, Bettina (DW Berlin)/Josephat Charo

Mhariri:Yusuf Saumu Ramadhani