1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Kikomunisti cha China chaanza mkutano mkuu

Mohammed Khelef
18 Oktoba 2017

Rais Xi Jinping amefungua mkutano mkuu wa chama chake, akitoa hotuba iliyochanganya matumaini ya uchumi kukua na vitisho kuelekea maeneo ambayo China inayatambua kuwa sehemu yake, ikiwemo Taiwan.

https://p.dw.com/p/2m3aX
China Peking Kommunistischer Parteitag Xi Jinping
Picha: Reuters/J. Lee

J3China: Communist party congress - MP3-Stereo

Akiwahutubia wajumbe 2,300 kwenye ufunguzi wa mkutano huo hivi leo, Rais Xi Jinping alisema mfumo wa ujamaa wa China sasa umeingia kwenye zama mpya, ambazo zina mchanganyiko wa changamoto na fursa, lakini akiwahakikishia kuwa taifa hilo la pili kwa ukubwa wa uchumi duniani liko kwenye njia sahihi kuelekea mafanikio yake.

"Hali ndani ya nje ya nchi yetu inapitia kwenye mabadiliko makubwa na changamano sana. Maendeleo ya China bado yapo kwenye hatua ya fursa muhimu za kimkakati. Huko mbele tuendako ni kuzuri sana, lakini nazo  changamoto za kutufikisha huko ni kubwa pia."

Xi ametumia kaulimbiu yake ya "Ndoto ya China", akiapa kwamba nchi yake itashinda vita dhidi ya umasikini, huku akionya kwamba ataendelea na sera yake ya kutokuwa na huruma kwenye vita dhidi ya ufisadi.

Katika hotuba hiyo ya ufunguzi, Xi alizungumzia pia siasa za nje za China, ukiwemo mradi mashuhuri uliopewa jina la "Mkanda Mmoja, Barabara Moja", ambao unajumuisha uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ya kuifungulia njia China na kuiunganisha na Ulaya na Afrika.

Vitisho kwa Taiwan

Ingawa ilitegemewa, hoja ya siasa ya China kuelekea Taiwan, ambayo inaichukulia kuwa sehemu yake, aliizungumza kwa ukali na vitisho zaidi, akisema kuwa serikali kuu mjini Beijing itatumia nguvu na dhamira yake kusitisha jaribio lolote lile la kujitangazia uhuru.

China Peking Kommunistischer Parteitag
Wajumbe 2,300 kutoka kote nchini China wanahudhuria mkutano mkuu unaotazamiwa kumchagua tena Rais Xi Jinping kukiongoza Chama cha Kikomunisti kwa miaka mingine mitano.Picha: picture-alliance/ZumaPress/Lan Hongguang

"Hatutamruhusu yeyote, au kundi lolote, au chama chochote cha siasa, kwa wakati wowote na kwa namna yoyote, kuitenganisha sehemu yoyote ya mamlaka ya China na China."

Lakini muda mchache baada ya kauli hiyo, serikali ya Taiwan ilitoa taarifa ikisema kuwa ni haki ya raia milioni 23 wa Taiwan pekee kuamua mustakabali wao. "Ukuu wa mfumo wa kidemokrasia wa Taiwan ndio msingi mkuu wa maadili ya Taiwan," ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Baraza la Masuala ya Mambo ya Bara ya Taiwan, likijibu hotuba ya Rais Xi. 

Mahusiano baina ya pande hizo mbili yamezidi kuchafuka tangu kuchaguiwa kwa Tsai Ing-wen kuwa rais wa Taiwan mwaka jana. China ilikata mawasiliano rasmi na serikali ya Tsai kutokana na kukataa kwake kutamka hadharani imani yake kwa sera ya "China Moja, Mifumo Miwili" inayotambuliwa na serikali kuu mjini Beijing. 

Serikali iliyopita ya Taiwan, pande hizo mbili zilikubaliana kubakia na makubaliano ya mwaka 1992, ambayo yanakubali kuwa kuna China moja tu, bila ya kutaja ni upi hasa unaowakilisha China yenyewe. 

Xi anachukuliwa na wengi nchini China kuwa ndiye kiongozi mwenye ushawishi zaidi tangu zama za Deng Xianpong na au hata Mao Zedong, na wengi wanasema atautumia mkutano huu mkuu kujiimarisha zaidi kwenye chama cha kikomunisti chenye wanachama milioni 89 na kukaa zaidi ya kipindi cha kawaida cha miaka 10.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba