1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha marehemu Benazir Bhutto chakutana leo

Josephat Charo30 Desemba 2007

Chama cha Pakistan People´s Party chatafakari kujiondoa katika uchaguzi

https://p.dw.com/p/ChzF
Marehemu Benazir BhuttoPicha: AP

Chama cha Pakistan Peoples Party, PPP, kinakutana hii leo kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wake, waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto, ili kuamua ikiwa kitashiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini Pakistan tarehe 8 mwezi ujao wa Januari.

Chama cha PPP pia kitasikiliza wosia wa marehemu Bhutto, huku kukiwa na hali ya kutatanisha kuhusu kifo chake.

Serikali ya Pakistan imekataa msaada wa kigeni katika kuchunguza kifo cha Benazir Bhutto.

Kundi la wanamgambo wa kiislamu lililotajwa kuhusika na mauaji ya kiongozi huyo limepinga kuhusika na njama ya kumuua, na wapambe wa Benazir Bhutto wameilaumu serikali kwa kujaribu kufunika ukweli.

Kujiondoa kwa chama cha Pakistan Peoples Party kushiriki katika uchaguzi wa Januari 8 kutavuruga uhalali wa uchaguzi huo, ambao tayari umegomewa na chama cha kiongozi mwengine wa upinzani nchini Pakistan, Nawaz Sharif.

Wakati haya yakiarifiwa, Marekani imekataa kusema lolote juu ya uwezekano wa Pakistan kuahirisha uchaguzi uliopangwa kufanywa tarehe 8 mwezi ujao wa Januari, kufuatia mauaji ya waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto.

Msemaji wa rais George W Bush, Tony Fratto, amesema wapakistan wanatakiwa waamue wenyewe kulingana na hali ilivyo nchini humo baada ya kuuwawa kwa Benazir Bhutto.

Aidha msemaji huyo amesema uchaguzi huo unatakiwa uwe huru na wa haki na wagombea wanatakiwa waweze kuendesha uchaguzi kwa uwazi.

Tume ya uchaguzi nchini Pakistan imesema itafanya mkutano wa dharura hapo kesho Jumatatu kujadili uwezekano wa kuuahirisha uchaguzi kwa sababu ya vurugu zilizosababishwa na kifo cha Benazir Bhutto aliyeuwawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na mtu wa kujitoa muhanga maisha wakati alipokuwa akiondoka kutoka mkutano wa kampeni.

Watu takriban 30 wameuwawa na wengine 53 wamejeruhiwa kufuatia machafuko yaliyozuka nchini Pakistan tangu kuuwawa kwa Benazir Bhutto.