1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha MDC chasusia kushiriki maamuzi ya serikali Zimbabwe.

Sekione Kitojo17 Oktoba 2009

Marekani imeitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kumshinikiza rais Robert Mugabe kutekeleza makubaliano ya kugawana madaraka.

https://p.dw.com/p/K8r1
Waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai, kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC.Picha: AP

WASHINGTON:

Marekani imeitaka Jumuia ya Kimataifa kuendelea kumshinikiza Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kutekeleza makubaliano ya kugawana madaraka, wakati chama kinachoshiriki kuunda serikali ya nchi hiyo cha Movement for Democratic Change MDC, kikisusia shughuli za Baraza la mawaziri.

Akizungumza mara baada ya Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai kutangaza kusimamisha ushirikiano na Rais Mugabe, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Ian Kelly amesema wanaelewa jinsi upinzani ulivyovunjika moyo kutokana na kukosekana maendeleo ya utekelezaji makubaliano hayo.

Bwana Tsvangirai amesema wanajitoa kutoka kwa mshirika ambaye amedai kuwa si muaminifu na si wa kutegemewa.

Kauli hiyo ya Bwana Tsvangirai imekuja siku moja tu baada ya mmoja wa wanachama waandamizi wa chama cha MDC, Roy Bennet, kuwekwa kizuizini baada ya dhamana yake juu ya mashtaka yanayomkabili ya ugaidi kufutwa.

Hata hivyo Bwana Bennet ameachiliwa huru jana kwa dhamana.