1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha SPD chazindua mkakati wa kampeni zake

Zainab Aziz
2 Agosti 2017

Chama cha Social Democratic (SPD) nchini Ujerumani kimezindua mkakati wa kampeni zake ili kumpa upinzani mkali kansela Angela Merkel katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/2hXO3
Deutschland Berlin - SPD Generalsekretär Hubertus Heil präsentiert die neue Walkampfkampaqne
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Wakati zimebakia wiki chache kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani chama cha Social Democratic (SPD) kilichopo nyuma ya chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union (CDU) katika kura ya maoni, katibu wake mkuu Hubertus Heil ameuzindua mkakati wa kampeni za uchaguzi kwa kuzitangaza sera za msingi za chama chake kwenye mabango matano katika mji mkuu, Berlin.  Katibu mkuu huyo wa chama cha SPD alisema anataka chama hicho kiwe na nguvu ili mgombea wake wa Ukansela Martin Schulz ashinde katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 24, Septemba.

Mpango wa kampeni wa chama cha Social Democratic (SPD) uliogharimu kiasi cha Euro milioni 24 unafafanua sera tano za msingiambazo ni Familia, Elimu, Mafao ya Wastaafu, Teknolojia za Kisasa pamoja na mishara sawa kwa wanaume na wanawake.Akifafanua lengo la kampeni hiyo katibu mkuu wa chama cha SPD Hubertus Heil amesema wanataka chama cha SPD kitakachokuwa na nguvu katika siku ya uchaguzi ya tarehe 24 Septemba. Heil amesema wanampigania Martin Schulz ili ashinde katika uchaguzi na awe Kansela wa Ujerumani na pia wana imani kubwa kwamba haki ikizingatiwa katika nchini Ujerumani, kutakuwepo na mustakabali mzuri na kwa hivyo ameeleza kuwa kampeni hii ya uchaguzi inahusu kuleta fursa ya haki zaidi.

Deutschland Berlin - SPD Generalsekretär Hubertus Heil präsentiert die neue Walkampfkampaqne
Katibu mkuu wa chama cha Social Democtratic (SPD) Hubertus HeilPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Akisisitiza juu ya swala hilo la haki zaidi katibu mkuu wa chama cha SPD Hubertus Heil amesema anayefanya kazi kwa asilimia 100 ya nguvu zake hatapunjwa kwa kulipwa asilimia 21 pungufu.  Chama cha SPD pia kinataka mfumo wa elimu kwa wote bila ya malipo. 

Chama cha SPD ambacho kwa sasa kimo katika serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Angela Merkel kimeyaweka kando ya mabango maswala nyeti juu ya mgogoro wa wakimbizi na dhima ya Umoja wa Ulaya lakini katibu mkuu wa chama hicho amesema maswala hayo yatazungumziwa wakati wa kampeni za uchaguzi. 

Bwana Heil amefahamisha kwamba kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz atakayegombea ukansela ataanza ziara ya nchini Ujerumani kote baadaye mwezi huu. Lakini atapaswa kuruka kiunzi kirefu kwa sababu kura za maoni zinaonyesha chama cha SPD kipo nyuma ya chama cha CDU kwa asilimia kati ya 14 na 18.

Mwandishi: Zainab Aziz/dw.com/p/2hW2Y

Mhariri:Josephat Charo