1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Afrika Kusini ANC kuchaguwa uongozi wake leo

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CcTY

POLOKWANE

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC leo kinapiga kura kuchaguwa uongozi wake baada ya kuahirishwa hapo jana uchaguzi ambao unatazamiwa kuwa wa mchuano mkali ambao unaweza kumsafishia njia naibu tata wa chama hicho Jacob Zuma kuja kuwa rais wa Afrika Kusini.

Zuma ambaye ni mashuhuri miongoni mwa vyama vya wafanyakazi na wanawake pamoja na wanachama wa kawaida wa chama hicho anatazamiwa sana kunyakuwa wadhifa huo kutoka kwa Mwenyekiti mtetezi Thabo Mbeki wakati wanachama 4,000 watakapopiga kura leo hii katika mji wa Polokwane na ambapo matokeo yake pia yanaweza kujulikana leo hii.

Katika kile kinachoonekana kama kujibu mapigo ya kutaka kumn’gowa kweye wadhifa huo Mbeki akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama hicho amemshambulia kwa njia isio wazi mpinzani wake mkuu na naibu wake wa chama Zuma aliekumbwa na kashfa kwa kuwataka wanachama wamchaguwe mtu mwenye maadili.

Mbeki ameonya kwamba rushwa,matumizi mabaya ya madaraka na mgawanyiko uliomo ndani ya chama unatishia kukiangamiza chama hicho cha ANC.

Mbeki anasema iwapo wamegawika wanapaswa kufanya nini kushughulikia changamoto hiyo kwa kuzingatua ukweli ulio wazi kwamba chama cha ANC kilichogawika hakiwezi kamwe kutekeleza majukumu yake ya kihistoria kwa umma wa wananchi.

Juu ya kwamba lazima ajiuzulu urais wa Afrika Kusini hapo mwaka 2009 Mbeki anataka kuendelea kukidhibiti chama hicho ili kuhakikisha kwamba anaweza kuongoza bila udhia wakati wa muda wake uliobakia madarakani kadhalika asaidie kumchaguwa na kumuongoza mrithi wake.

Chama cha ANC kimeitawala Afrika Kusini tokea kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo hapo mwaka 2004.