1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Burundi chatarajiwa kushinda kwa kishindo

1 Julai 2015

Maafisa wa tume ya uchaguzi ya Burundi wamekamilisha kuhesabu kura Jumanne (30.06.2015) huku chama tawala wa CNDD-FDD kikitarajiwa kushinda kwa kishindo uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa.

https://p.dw.com/p/1Fr78
Parlamentswahlen in Burundi
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Ngingo

"Uhesabuji wa kura umekamilika katika vituo vyote vya kupigia kura kote Burundi," alisema msemaji wa tume ya kitaifa ya uchaguzi CENI, Prosper Ntahorwamiye, wakati alipozungumza na shirika la habari la AFP, huku kura hizo zikikusanywa na kupelekwa katika vituo vikubwa ili zijumuishwe mara ya mwisho kabla matokeo kutangazwa.

Upigaji kura siku ya Jumatatu uligubikwa na mashambulizi ya maguruneti huku tume ya uchaguzi ikidai idadi kubwa ya wapigaji kura walijitokeza licha ya vituo vingi kutokuwa na shughuli nyingi.

Uchaguzi huo ulifuatia wiki kadhaa za machafuko na jaribo la mapinduzi lililofeli, ambalo lilisababishwa na nia ya rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kugombea awamu ya tatu madarakani, huku watu zaidi ya 70 wakiuliwa.

Watu takriban milioni nne walisajiliwa kupiga kura lakini upinzani uliugomea uchaguzi huo kama ulivyofanywa katika chaguzi za mwaka 2010, ukidadi haikuwezekana kufanya uchaguzi huru na wa haki. Wakimbizi wapatao 144,000 wameihama Burundi na kukimbilia mataifa jirani.

Waangalizi pekee wa kimataifa katika uchaguzi huo walikuwa wa Umoja wa Mataifa ambao walisema kuwepo kwao Burundi kusitafsiriwe kama uhalalishaji wa mchakato mzima wa uchaguzi. Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki Moon awali alitoa mwito uchaguzi ucheleweshwe huku Burundi ikikabiliwa na mzozo wake mbaye kabisa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka tisa iliyopita.

Warundi waikimbia nchi

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, limesema Warundi takriban 10,000 wameikimbia nchi yao mwishoni mwa juma lililopita kabla serikali mjini Bujumbura kufunga mipaka yake wakati uchaguzi huo wenye utata ulipokuwa ukisubiriwa. Shirika hilo lilisema watu wapatao 144,000 wamekimbia Burundi tangu mwezi Aprili mwaka huu wa 2015 wakati machafuko ya kisiasa yalipoanza.

Tansania Flüchtlinge aus Burundi
Wakimbizi wa Burundi nchini TanzaniaPicha: Reuters/T. Mukoya

Umoja wa Afrika ulikataa kupeleka waangaliziu wake kwa sababu haikuwezekana kufanya uchaguzi huru, wa haki, wa uwazi na halali.

Umoja wa Ulaya ulionya uchaguzi huo ungechochea mzozo uliopo hivi sasa, huku mkoloni wa zamani wa Burundi, Ubelgiji, ikisema uchaguzi huo haukuwa halali na yumkini ukaligawa zaidi taifa.

Kwa mujibu wa msemaji wa tume ya kitaifa ya uchaguzi, Prosper Ntahorwamiye, matokeo ya awali ya uchaugzi wa serikali za mitaa yalitarajiwa kukamilika Jumanne jioni au Jumatano, wakati matokeo ya uchaguzi wa bunge yanapotarajiwa kutangazwa. Ntahorwamiye aliongeza kusema haiwezekani kutoa idadi kamili ya wapigaji kura waliojitokeza kutumbukiza kura zao vituoni kabla matokeo kukamilishwa.

Awamu ya kwanza ya uchaguzi yakamilika

Jumanne jioni rais Nkurunziza aliitaka jumuiya ya kimataifa iuheshimu uhuru wa Warundi akiongeza kuwa uchaguzi ulikuwa umefanyika vyema.

Uchaguzi wa bunge na wa serikali za mitaa siku ya Jumatatu ni awamu ya kwanza ya chaguzi tatu Burundi, huku uchaguzi wa rais ukiwa umepangwa kufanyika Julai 15 ukifuatiwa na uchaguzi wa maseneta Julai 24 mwaka huu.

nach Putschversuch - Präsident Pierre Nkurunziza zurück im Amt
Rais Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Wapinzani wanasema azma ya rais Nkurunziza kugombea awamu ya tatu ni kinyume na katiba na inakiuka mkataba wa amani wa Arusha uliovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2006 vilivyodumua miaka 13. Mashirika ya kijamii yaliunga mkono hatua ya kuususia uchaguzi katika taarifa ya pamoja iliyowataka wapigaji kura wasishiriki uchaguzi huo bandia.

Kwa mujibu wa katiba na kwa kuzingatia mikataba ya amani iliyovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, kuna utaratibu wa idadi ya wabunge inayotakikana bungeni kutoka makabila yote. Bunge lazima liwe na asilimia 60 ya wabunge kutoka kwa jamii ya Wahutu walio wengi, ambao ni asilimia 85 ya idadi ya wakazi Burundi, huku asilimia 40 ya viti bungeni vikitengewa jamii ya Watutsi walio wachache.

Kiongozi wa upinzani Pacifique Nininahazwe, aliyeandaa maandamano ya kuipinga serikali kabla kukimbilia uhamishoni, alisema serikali ya Burundi huandaa takwimu za uongo.

Kiongozi mwenzake wa upinzani Charles Nditije alisema chaguzi za Jumatatu ni mchezo wa kuiga kwa kubeza.

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri:Iddi Sessanga