1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League Ulaya na Afrika kutimua vumbi Jumanne

Sekione Kitojo
26 Novemba 2018

Champions League, timu mbali mbali kuwania kufuzu kuingia katika duru ya mtoano katika mapambano ya Jumanne na Jumatano. Na barani  Afrika, ligi ya mabingwa  kutimua  vumbi pia Jumanne  na  Jumatano.

https://p.dw.com/p/38w1x
Kylian Mbappe
Mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe, anatarajiwa kurejea uwanjani kupambana na LiverpoolPicha: picture-alliance/abaca/H. Szwarc

Katika  Champions League  barani  Ulaya vigogo vya  soka  vingi  katika  barani  la Ulaya  vinahitaji  pointi  moja  tu kujihakikishia  kuingia  katika  duru  ya  mtoano, lakini mbinyo  wa Champions League  unaikabili  zaidi Paris Saint-Germain  na  Tottenham, wakati  Bayern  Munich ikihitaji  kwa  udi  na  uvumba  msukumo zaidi. Vigogo  vingi  vitakuwa  na  matumaini  kesho  na  keshokutwa kujiunga  na  Barcelona   katika  timu  16  zinazobakia  katika Champions  League , wakati  nyingine  zikitaraji  kuepuka kuondolewa.

UEFA Champions League | Paris St Germain vs. Crvena Zvezda Thomas Tuchel
kocha wa PSG Thomas Tuchel akabiliwa na mbinyo mkali kuweza kuvusha timu yake kuingia katika duru ya mtoanoPicha: Getty Images/AFP/A. Poujoulat

Mabingwa  wa  Ulaya  Real Madrid, Manchester City, Bayern Munich , Roma, Juventus, Inter Milan  na  Porto  zote  zinahitaji pointi  moja  katika  awamu  hii  ya  makundi  kufuzu.

Baadhi  ya  timu  nyingine  zitakuwa  na  matumaini  ya  kukata tikiti zao  kwa  ushindi, wakati  timu  kama  Paris Saint-Germain , Tottenham Hotspur  na  Valencia  zinapambana  na  hali  zao.

Kundi  C ni  moja  kati  ya  makundi  ambayo  timu  zinakaribiana sana  ambako  Napoli itafuzu  iwapo itaishinda  Red Star Belgrade na  PSG itashindwa  kuiangusha  Liverpool.

Hiyo  ndio  hali  ya  mambo  katika  kinyang'anyiro  hicho ambapo kikosi  cha  Juergen Klopp  kinatarji  kukamilisha  hatua  hiyo  kwa ushindi  mjini  Paris  iwapo  Napoli  itaepuka  kushindwa, lakini  PSG , ambayo  inamatumaini  ya  kuongezewa  nguvu  na  wachezaji wake  wa  kati Neymar  na  mshambuliaji Kylian  Mbappe , watakuwa wakipigania  maisha  yao.

UEFA Champions League | Paris Saint-Germain vs. Roter Stern Belgrad
Mshambuliaji wa PSG Neymar akipambana na mlinzi wa Red Star Belgrade BrankoPicha: Getty Images/AFP/F. Fife

Vigogo vya  Afrika

Katika  Bara   la  Afrika  kuna  mabingwa  wa  zamani  watano  wa Champions League  barani  humo  miongoni  mwa  timu  52 zinazohusika  katika  kinyang'anyiro  cha  msimu  wa  mwaka  2018 / 19 kesho  Jumanne  na  Jumatano. Orlando Pirates  ya  Afrika kusini  na  ASEC Mimosas  ya  Cote d'Ivoire  zinaanza  duru  ya mwanzo  kwa  michezo  ya  nyumbani.

Ismailia  ya  Misri , Mamelodi Sundowns  ya  Afrika kusini  na  Club Africain  ya  Tunisia zina changamoto  kubwa  wakati  zinasafiri kwenda  katika  mapambano  yao. Mabingwa  wengine  watano mabingwa  watetezi Esperance  ya  Tunisia, TP Mazembe  na  V Club  za  Jamhuri  ya  kidemokrasi  ya  Congo, Al Ahly  ya  Misri  na Wydad Casablansa  ya  Morocco  zimepita   na  kuingia  katika  duru ya  pili.

Fußball | Afrikanische Champions League | Esperance Tunis gewinnt Titel
Wachezaji wa Esperance ya Tunisia wakishangiria ushindi wa Champions League barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya MisriPicha: Reuters/Z. Souissi

Simba  ya  Tanzania  inakwaana  na  Mbabane Swallows  ya Eswatini  zamani  Swaziland, wakati Gor Mahia  ya  Kenya  iko nyumbani  ikiisubiri  Big Bullets  ya  malawi. nayo  Al Merrikh  ya Sudan  ni  wenyeji  wa  Vipers  ya  Uganda. Al Hilal  ya  Sudan inapambana  na  JKU  ya  Zanzibar.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe /rtre / ape / dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman