1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto kali zamkabili Condoleezza Rice

P.Martin20 Oktoba 2007

Mzozo juu ya ajenda ya mkutano kuhusu suala la kuundwa taifa la Palestina,huashiria kazi ngumu inayomngojea Waziri wa Nje wa Marekani Condoleezza Rice,pale Wapalestina na Waisraeli watakapoanza kujadiliana rasmi.

https://p.dw.com/p/C7gq

Juhudi za kidiplomasia za Bibi Rice wakati wa ziara yake ya siku nne katika Mashariki ya Kati, hazikutosha kupunguza tofauti za maoni kati ya Waziri Mkuu wa Israel,Ehud Olmert na Rais wa Wapalestina,Mahmoud Abbas.Viongozi hao hawakuweza kuafikiana kuhusu hati ya pamoja wanayotazamia kuiwasilisha kwenye mkutano utakaofanywa mwezi Novemba au Desemba nchini Marekani.

Hata ikiwa maafikiano yatapatikana kuhusu hati hiyo,changamoto nyingine kubwa inayomkabili Condoleezza Rice ni kuwakutanisha Olmert na Abbas kwa majadiliano rasmi ya kuunda taifa la Palestina na kujaribu kupata makubaliano kabla ya Rais George W.Bush kuondoka madarakani.Huo ni mtihani mkubwa mno.

Kwani masuala mengi yanayopaswa kukubaliwa na Olmert ili kuweza kuafikiana na Abbas,kama kuugawa mji wa Jerusalem na maeneo takatifu katika mji huo,hadi kuhamisha Wayahudi kutoka Ukingo wa Magharibi uliokaliwa na Israel-ni masuala yanayoweza kuiangusha serikali ya mseto nchini Israel na uchaguzi mpya kuitishwa nchini humo.Hatua hiyo huenda ikakwamisha utaratibu wa amani hadi Bush kumaliza awamu yake.

Hata Abbas,aliepoteza Ukanda wa Gaza baada ya wapiganaji wa Hamas kudhibiti eneo hilo, atakabiliwa na hali ngumu ikiwa majadiliano hayo yatakwama.Chama cha Hamas ndio kitaimarika na uaminifu wa Marekani utazidi kudhoofika.

Vile vile maafisa wa Kiisraeli na Kipalestina wanahofu kuwa machafuko yatazuka upya ikiwa majadiliano ya safari hii hayatofanikiwa.

Wakati huo huo waziri Rice amesema,wapatanishi wa hivi sasa wanapswa kujitahidi zaidi kutenzua matatizo yaliyokuwepo-kama vile masuala ya mipaka,hadhi ya mji wa Jerusalem,wakimbizi wa Kipalestina na makaazi ya Wayahudi.

Olmert ameashiria kuwa yeye yupo tayari kufikiria kutoa kama asilimia 90 ya Ukingo wa Magharibi, lakini suala linaloulizwa ikiwa yutayari pia kurejesha sehemu yote ya Gaza kama iliyopendekezwa na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton?

Kwa maoni ya afisa mmoja wa Kiisraeli wa ngazi ya juu,anaehusika na majadiliano ya hivi sasa, majadiliano kati ya Abbas na Olmert yanalenga kuwaimarisha viongozi hao wawili na kuvunja nguvu za maadui wao.

Anasema,Olmert anajitahidi kujitetea dhidi ya mahasimu wake wa kisiasa kufuatia vita vya mwaka jana nchini Lebanon.Abbas nae anatazamia kujiimarisha mbele ya Hamas.Kwa upande mwingine Rais Bush na Bibi Rice kabla ya kuondoka madarakani,wanataka kungárisha urithi wao kufuatia vita vya Iraq.Vile vile wanataka waungwe mkono na Waarabu kuhusu suala la Iran.