1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Kimataifa ya Ulemavu wa Ngozi

13 Juni 2015

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Ulemavu wa Ngozi. Makundi ya haki yameongeza kampeni kuhusu masaibu ya watu wenye ulemavu huo. Katika nchi kama Tanzania, watu hao wanakabiliwa na vitisho vya kuuliwa kwa imani za kishirikina

https://p.dw.com/p/1Fgav
Symbolbild Albinos in Afrika
Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Mohamed Mabula anaitunza familia kwa kupitia biashara ndogo ya bodaboda ya baiskeli katika kijiji cha Ndembezi, kaskazini mwa Tanzania. Kawaida fedha ni vigumu kupatikana na kutosha kwa sababu wawili kati ya watoto wake sita wanahitaji ulinzi maalum. Shija mwenye umri wa miaka minne na Dotto mwenye umri wa miaka sita wana ulemavu wa ngozi, yaani albino. Ni hatari sana kuishi Tanzania ukiwa na hali hii.

Sababu ni imani potofu za kishirikina zinazoenezwa na wafanyabiashara na waganga wa kienyeji. Wanaamini mazeruzeru wana nguvu za kichawi. Wanasema dawa maalum zinaweza kupatikana kutoka kwenye mifupa yao.

Tansania Albino Mutter und Kind
Wengi wanawachukulia watoto wenye ulemavu wa ngozi kuwa ni laana katika jamiiPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Kwa mujibu wa watalaamu, viungo vya miili ya watu wenye ulemavu wa ngozi huuzwa kwa mamilioni ya shilingi kwenye soko la magendo na watu wanaweza kuuzwa wakiwa hai au wamekufa kwa hadi euro 65,000. Hiyo ndio maana maalbino aghalabu hujikuta kuwa wahanga wa mashambulizi. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa takribani watu 75 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa nchini Tanzania tangu mwaka 2000, huku wengine wengi wakikatwa viungo vyao.

Vita dhidi ya imani za kishirikina

Kutokana na idadi kubwa ya mashambulizi ya maalbino mwaka huu, serikali ya Tanzania imefanya misako, ambapo zaidi ya waganga wa kienyeji 200 walikamatwa na kuzuiliwa. Rais Jakaya Kikwete akizungumza mwezi Machi alilaani mashambulizi hayo “kuwa ya kuchukiza na aibu kwa nchi”.

Mashirika kadhaa kama vile Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi nchini Tanzania yanafanya kazi kuwalinda maalbino. Kupitia michango, yanaeneza ujumbe na uelewa na pia kutoa mazingira bora ya kuishi mazeruzeru. Juhudi zao zianonekana katika maeneo tofauti nchini humo. Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Valentino Mlolowa ameiambia DW kuwa hali ya mazeruzeru kati ya 2006 na 2009 ilikuwa mbaya katika eneo hilo. Lakini tangu 2010, imeimarika baada ya kuripotiwa kisa kimoja pekee cha kushambuliwa albino.

Tansania Albino Kinder
Walemavu wa ngozi Tanzania wanahifadhiwa katika vituoPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Mlolowa anahisi kuwa hatua kama vile mipango ya serikali katika shule za wilaya ni muhimu. Anasema lengo la mipango hiyo ni kuimarisha somo la bayolojia. Wanafunzi hupewa mafunzo kuwa ulemavu wa ngozi unatokana na urithi na hauna uhusiano na uchawi. Mlolowa anasema ushirikina utapungua ikiwa kutakuwepo na elimu ya kutosha ya sayansi.

Hakuna maisha bila ya hofu

Licha ya juhudi hizi zote, yapo mengi ya kufanywa ili kuwapa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania maisha bora. Familia nyingi bado zinawaficha watoto wao wenye hali hiyo. Wengine wanaishi katika vituo maalum ambako wanaweza kupewa elimu na kulindwa kama vile shule ya msingi ya Mazoezi Kabanga mjini Kigoma, magaribi mwa Tanzania.

Lakini kwa Hamida Ramadhani, mama wa watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi, hili siyo suluhisho la muda mrefu. Anajihisi ni kama amewekwa kizuizini katika kituo cha Kigoma na kutengwa na jamii.

Deborah Ruge mwenye umri wa miaka 14 pia anaishi katika kituo hicho. Tangu mwaka wa 2010, watu wasiojulikana wamekuwa wakijaribu kumuua. Hata ingawa anahisi kutunzwa vyema kituoni humo, Ruge anasema anatamani sana kuwa na familia yake.

Tansania Albino Frau Mädchen
Maalbino hushambuliwa kwa sababu za kishirikinaPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/J. Martin

Berthold Alfred, ni mwalimu wa shule ya msingi. Wazazi wake, wanaoishi katika kijiji karibu na mpaka wa Burundi, hawajamtembelea kwa muda sasa. Anahisi msaada wake unahitajika sana nyumbani.

Mlemavu wa ngozi bungeni

Watu wenye ulemavu wa ngozi wanaweza kutoa mchango mkubwa sana katika kuimarisha uwepo wao katika jamii na kusaidia kupunguza chuki na ubaguzi dhidi yao. Isaac Mwaura anaishi na hali hiyo na ni mbunge nchini Kenya. Anasema aliwasilisha bungeni mswaada ambao ulipendekeza hukumu ya kifungo cha maisa gerezani kwa yeyote anayehusika na mauaji ya albino. Kupitia shirika lake la Chama cha Maalbino nchini Kenya, Mwaura amechangisha shilingi milioni 100 (900,000) ili kuwasaidia walemavu wa ngozi. Anasema fedha hizo hutumiwa kununua krimu za kujipaka kwenye ngozi ili kuzuia miale ya jua, miwani ya jua na kofia.

Mwandishi: Bruce Amani/Philip Sandner
Wachangiaji: Bruce Amani, Amina Abubakar, Prosper Kwigize, Veronica Natalis
Mhariri: Mohammed Khelef