Changamoto ya usalama ni kitisho duniani
17 Februari 2018Viongozi na wakuu wa nchi pamoja na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi mbali mbali za dunia wanaendelea na mkutano wao muhimu juu ya usalama wa dunia katika mji wa Munich hapa Ujerumani. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel aliyezungumza leo Jumamosi kwenye mkutano huo ameonya kwamba ulimwengu unakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama pamoja na kitisho cha kuzuka migogoro mikubwa katika kanda mbali mbali.
Waziri huyo amesema kwamba ubashiri wa mambo na uhalisia ni masuala yaliopo katika siasa za kimataifa,huku akiongeza kusema kwamba mgogoro wa Syria unaelekea mahala kunakoonesha hatari kubwa ya kuzuka vita katika upande wa washirika wao wa karibu. Suala la mgogoro wa Korea Kaskazini limetawala mkutano huo ambapo pia waziri Gabriel amegusia kwamba kitisho kikubwa kinajitokeza katika mgogoro huo na hasa kwa kuzingatia nia ya China ya kutaka kuwa na dhima kubwa katika suala hilo,lakini juu ya hilo pia ni Urusi kutumia nguvu zake za kijeshi pamoja na kuongezeka kwa siasa za kizalendo na siasa za ubepari yote hayo yanasababisha kitisho kikubwa duniani.
Kwa upande mwingine Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ambaye nchi yake inajiandaa kuuaga Umoja wa Ulaya ametowa mwito mbele ya mkutano huo wa kutafutwa mkataba mpya na Umoja wa Ulaya utakaosimamia usalama kufikia mwaka ujao ili kuhakikisha muendelezo wa ushirikiano wa kijeshi,kiintelijensia na mapambano dhidi ya ugaidi baada ya nchi hiyo kujiondoa kabisa katika Umoja wa Ulaya. Theresa May anasema ushirikiano wanaouhitaji ni ule ambao utatoa fursa kwa Uingereza na Umoja wa Ulaya ya kupata njia ya kuunganisha juhudi zao kuwa na ufanisi mkubwa pale panapohusika maslahi ya pande zote.
Kadhalika kwenye mkutano huo unaomalizika Jumapili viongozi wa Umoja wa Mataifa pamoja na Jumuiya ya Kujihami NATO wamesisitiza haja ya kusuluhisha mgogoro unaohusu silaha za kinyuklia wa Korea Kaskazini katika hotuba zao. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anthonio Guterres ametoa wito wa kuutaka mgororo huo upatiwe suluhisho kwa njia za kidiplomasia akisisitiza kwamba hatua za kijeshi zitasababisha maafa na matokeo mabaya.
"Ni muhimu kabisa kuendelea kuishinikiza Korea Kaskazini na kuishawishi kuja katika meza ya mazungumzo ili kuweza kupata njia ya kusitisha utengenezaji wa silaha za kinyuklia. Kuondoa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea inawezekana."
Mbali na wasiwasi juu ya silaha za nyuklia, Guterres alionya kwamba changamoto nyingine za usalama bado zimebaki kuwepo kwa kiwango kikubwa. Katibu Mkuu huyo alisema migogoro inayoendelea katika Mashariki ya Kati kama vile vita vya nchini Syria vinasababisha madhara hata nje ya kanda hiyo, kupitia ugaidi wa kimataifa au wingi wa idadi ya watu waliokimbia makazi yao wakikimbilia barani Ulaya na mahali pengine ulimwenguni. Kadhalika katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg aliyezungumza katika mkutano huo amerudia wito wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa kusema shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini lazima liendelezwe. Stoltenberg aliongeza kwamba Urusi na China zina wajibu kama nchi wanachama wa Baraza la Usalama na kama majirani wa karibu wa Korea Kaskazini.
Mwandishi: Saumu Yusuf/afp/Reuters
Mhariri: Jacob Safari