1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chelsea na Bareclona kuamua nani wa kukumbana na MANU fainali

Aboubakary Jumaa Liongo6 Mei 2009

Baada ya hapo jana Arsenal kufurushwa nje na Manchester United katika nusufainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, leo ni zamu ya Chelsea na Barcelona.

https://p.dw.com/p/Hkov


Chelsea leo hii inaikaribisha Barcelona katika mechi ya marudiano, huku ikitegemewa kushambulia zaidi kuliko kujihami kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza iliyomalizika bila ya mtu kuufumania mlango wa mwenzie.


Chelsea inajiwinda kukata tiketi yake ya fainali kwa mara ya pili mfululizo, huku Barcelona nayo ikitaka kuepuka mzimu wa kutolewa mara ya tatu mfululizo katika michuano hiyo na timu za Uingereza.


Mwaka jana Barcelona waliondoshwa na Manchester United, iliyosonga mbele hadi kutwaa ubingwa mbele ya Chelsea katika fainali.Na mwaka mmoja kabla ya hapo yaani mwaka 2007, Bacca walitimuliwa na Liverpool.


Umri wa wachezaji wa Chelsea umekuwa ukichukua nafasi katika mijadala kuelekea mechi hiyo ya leo, ambapo wengi wa wachezaji wake muhimu hivi sasa wana umri kuanzia miaka 30.


Guus Hiddink pamoja na kwamba ni kocha wa mpito , lakini ana usemi katika uamuzi wa nani abakie katika kikosi hicho msimu ujayo.


Fußball FC Barcelona Chelsea FC
Didie Drogba mbele akikabiliwa na beki wa Barcelona Gerard PiquePicha: picture-alliance / dpa

Ni dhahiri kabisa kuwa huenda kukawa na mabadiliko, kwahivyo mechi hiyo ya leo itakuwa ni nafasi ya mwisho kuthibitisha uwezo katika ushirikiano wa Michael Ballack ambaye ana miaka 32, Didier Drogba miaka 31, Lampard na Anelka wenye miaka 30 kila mmoja, na kuipatia ushindi timu yao.


Chelsea imefanikiwa kufika hatua ya nusufainali ya ligi hiyo mara tano katika kipindi cha miaka sita iliyopita, na kocha Hiddink anasema kuwa hii ni nafasi pekee kwa wachezaji hao kufika pale ambapo wanataka kufika nako ni kutwaa ubingwa.


Amesema kuwa wana hamu kubwa ya kutwaa ubingwa, lakini akasema unapocheza na timu kama Barcelona ni lazima uwe na akili za ziada kuweza kushinda.


´´Ni lazima ucheze kwa kutumia akili sana, unapokumbana na timu ambayo kiwango chake ni cha juu kabisa barani Ulaya kwa sasa.Kosa dogo tu litakugharimu, na kwa upande mwengine nadhani bilashaka huwezi kucheza bila ya jazba ambazo zinaweza kuathiri uchezaji wako, lakini iwapo utachanganya vitu hivyo viwili basi utakuwa na nafasi nzuri ya kushinda´´


Kufuatia matokeo ya bila kufungana katika mechi ya kwanza Barcelona imekuwa ikiulamu mbinu za Chelsea na kuishutumu kwa kutumia nguvu zaidi, kama anavyosema beki wa timu hiyo Silvinho


´´Mechi ya kwanza ilikuwa ngumu sana na tunategemea tena leo.Tunajua Chelsea ni timu yenye kutumia nguvu sana pamoja na ufundi pia, lakini mechi ya marudiano itakuwa mechi tofauti na ile ya kwanza´´.


Barcelona inaingia uwanjani ikiwa na hamasa ya ushindi mzito katika ligi ya nyumbani kwao dhidi ya mahasimu wao Real Madrid mwishoni mwa wiki ambapo iliishindilia mabao 6-2.


Lakini kocha wa Chelsea Hiddink ana hakika kuwa atawabana, Lionel Messi, Thierry Henry na Samuel Eto´o, akisema kuwa mazingira ya mechi ya leo ni tofauti na ya ligi ya ndani.


Amejivunia kiwango cha uchezaji alichofikia hivi sasa nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack, akisema ana hamu kubwa ya kukumbana na Manchester United katika fainali na kushinda kikombe.


Champions League Arsenal London Manchester United
Wachezajai wa Manchester United wakishangilia ushindi dhidi ya ArsenalPicha: AP

Hapo jana Manchester United ilipata kile kilichoonekana kama mteremeko ilipoifurusha Arsenal kwa kuichapa mabao 3-1 na hivyo kuingia fainali kwa jumla ya mabao 4-1.


Kufungwa kwa Arsenal kumesababisha shabiki mmoja wa timu hiyo jijini Nairobi nchini Kenya kujinyonga.


Shabiki Suleiman Alphonso Omondi mwenye umri wa miaka 29 anayeishi eneo la Embakasi nje kidogo ya Nairobi, huku akiwa na fulana ya Arsenal aliamua kukatisha maisha yake na kwenda kuzimu kutokana na uchungu wa kufungwa.


Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman