1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China kuimarisha ushirikiano na Afrika

23 Julai 2018

Rais wa China Xi Jin Ping amesema nchi yake imejizatiti kuimarisha ushirikiano wake na bara la Afrika kutokana na hatua ya maendeleo inayoendelea kuonekana barani humo.

https://p.dw.com/p/31wZo
Ruanda Besuch Präsident Xi Jinping China
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Rais Xi Jin Ping ameyasema hayo alipokuwa akizungumza mjini Kigali akiwa katika ziara ya siku mbili nchini Rwanda. Wakati huo mikataba kadhaa imesainiwa baina ya China Rwanda. Rais wa Uchina Xi Jin Ping yuko ziarani nchini Rwanda pamoja na mkewe na ujumbe mkubwa anaouongoza ukiwemo wawekezaji na viongozi wa serikali yake. Mapema leo alipokelewa kwa heshima na mwenzake RaisP Paul Kagame katika Ikulu mjini Kigali.

Mikataba mitano yasainiwa

Ruanda Besuch Präsident Xi Jinping China
Rais Xi Jinping akikagua gwaride na mwenyeji wake rais KagamePicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Baadaye viongozi hao wawili waliongoza zoezi la kutia saini mikataba kumi na mitano baina ya China na Rwanda kwenye Nyanja mbalimbali ikiwemo miundo mbinu ya barabara, sekta ya afya, elimu pamoja na diplomasia. Ktk diplomasia wanadiplomasia wa pande wameondolewa visa kwenda au kutoka ktk nchi moja kwenda nyingine.

Kwenye mkataba huu pia China imekubali kupanua barabara ya kilomita zaidi ya 40 kwa kiwango cha lami kutoka jijini Kigali kuelekea upande wa mashariki mwa nchi ambako serikali ya Rwanda inajenga uwanja mkubwa wa ndege utakaopokea zaidi ya wasafiri milioni 5 kila mwaka baada ya awamu ya kwanza ya uwanja huo kukamilika.

China inajivunia mahusiano na Afrika

Ruanda Besuch Xi Kinping Paul Kagame
Marais Kagame na Xi Jinping nchini RwandaPicha: picture-alliance/AP Photo

Akizungumza kupitia mkalimani mara baada ya zoezi hilo la kutia saini mikataba hiyo Rais Xi Jin Ping amesema kwamba serikali yake inajivunia uhusiano uliopo baina ya China na Rwanda pamoja na bara la Afrika ujumla akibaini umuhimu wa ziara yake nchini Rwanda."Hii ni ziara ya kihisitoria,ni ziara ya kwanza ya Rais wa China nchini Rwanda. Ninapoitazama Rwanda naiona nchi yenye utawala imara,nchi yenye watu wanaofurahia nchi yao. Niko hapa kuhakikisha tunadumisha uhusiano huu lakini zaidi kuzidisha uhusiano na bara la Afrika ili kuhakikisha wananchi wa pande mbili wanapata faida kutokana na uhusiano huu," Xi Jin Ping.

Rais Paul Kagame akizungumza pia amesema kwamba kutia saini kwa mikataba hii kumi na mitano ni ishara tosha kwamba uhusiano wa China na Rwanda pamoja na nchi nyingine za kiafrika unazidi kupiga hatua kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali "Hakika utiaji saini mikataba hii ni ishara tosha kuhusu kile kinachowezekana baina ya Rwanda na China pamoja pia na uhusiano wa China na bara la Afrika."

Rais Paul Kagame ambaye pia kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amezungumzia kwuhusu jinsi uhusiano huu usivyoishia kwa Rwanda tu lakini pia nchi nyingine za kiafrika zinavyoweza kufaidi ya uhusiano huu wa China nchi za kiafrika.

Baadaye viongozi hao wawili na ujumbe wanaoungoza wamekutana kwa dhifa maalum ambapo kwa ajili ya chakula cha mchana kabla ya Rais Xi Jin Ping kusafiri kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kikao cha mataifa matano yanayoinukia kiviwanda maarufu kama BRICS ikiwa ni pamoja na Brazil,India,Urusi, China na Afrika Kusini. Kwa upande mwingine hadi tulipokuwa tunaingia hewani alikuwa akisubiriwa pia waziri mkuu wa India Narendra Modi pia kwa ziara ya siku mbili nchini Rwanda.

Mwandishi: Sylvanus Karemera - DW Kigali

Mhariri: Iddi Ssessanga