1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Iran zapinga ripoti kuhusu hukumu ya kifo

Mwakideu, Alex15 Aprili 2008

China inaongoza katika orodha ya nchi zilizowauwa watu wengi zaidi mwaka jana kutokana na hukumu ya kifo.

https://p.dw.com/p/DiSf
Rais wa Iran Mahmoud AhmadinejadPicha: AP

China imesimama kidete na kusisitiza kwamba haitaondoa hukumu ya kifo licha ya ripoti mpya shirika la kutetea haki za binaadamu Amnesty International inayoonyesha nchi hiyo ikiongoza kote duniani kwa idadi ya watu waliouwawa kufuatia hukumu hiyo.


Mahakama nchini Iran imelezea kugadhabishwa kwake na ripoti hiyo na kujitetea kwamba idadi ya waliiouwawa nchini humo kutokana na hukumu ya kifo ni chache mno.


Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeiweka wazi ripoti inayohusu hukumu ya kifo na watu waliouwawa mwaka uliopita kufuatia hukumu hiyo.


Ripoti hiyo iliyowekwa wazi hapo jana imezua hisia kali kwa nchi zilizotajwa hususan China na Iran.


Kwa upande wake China imesema badala ya kuondoa hukumu ya kifo, itapunguza idadi ya watu wanaohukumiwa kulingana na maovu waliyotenda.


Msemaji wa wizara ya nchi za nje nchini humo Bi Jiang Yu amesema nchi zinazotumia hukumu hiyo duniani ni nyingi zikilinganishwa na zile zisizoitumia.


Katika ripoti yake; shirika la Amnesty limesema China iliwauwa watu 470 mwaka uliopita. Hata hivyo idadi hiyo huenda ikawa ndogo kwani ripoti hiyo imeongezea kwamba serikali ya China imeweka siri idadi kamili ya waliouwawa.


Katika ripoti nyengine mwezi ulipita jaji mkuu wa China alitetea hukumu hiyo akisema inatolewa kwa njia ya haki na chini ya maelewano yaliyoafikiwa januari mwaka uliopita.


Iran ambayo inaifuata China katika orodha ya nchi zilizoitumia zaidi hukumu ya kifo mwaka uliopita imesisitiza kwamba idadi ya waliouwawa nchini humo sio kubwa.


Serikali za Ulaya na mashirika yakutetea haki za binadamu wameshutumu Iran kwa ongezeko la watu wanaonyongwa tangu nchi hiyo ilipoanzisha mpango wa kumaliza usharati mwezi July.


Katika ripoti yake shirika la Amnesty International limesema Iran iliwauwa watu 317 waliokuwa wamehumiwa kifo mwaka uliopita.


Msemaji wa mahakama nchini humo Alizera Jamshidi amesema idadi kubwa ya watu wanaohukumiwa kunyongwa nchini Iran inaweza kuondolewa na jamaa za aliehukumiwa kwa kulipa faini ya kiasi fulani.


Watuhumiwa wanaoshtakiwa kwa kuua, kuzini, kubaka, kuiba kwa kutumia silaha, kuiasi dini na kuuza madawa ya kulevya ndio wanaoweza kuhukumiwa kifo kwa mujibu wa sharia ya kiislamu ambayo imekuwa ikitumika nchini Iran tangu mwaka wa 1979 wakati nchi hiyo iliponyakuliwa na kugeuzwa kuwa nchi ya kiislamu chini ya utawala wa Ayatoll Ruhollah Khomeini.


Nchini China zaidi ya visa 70 vya uhalifu vikiwemo, kupokea hongo, na kuuza madawa bandia vinaweza kupelekea hukumu ya kifo.


Takriban watu 1, 252 waliuwawa mwaka jana katika nchi 24 na wengine 3,347 walihukumiwa kifo katika nchi 51.


Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema China na Iran zinafuatiwa na Saudi Arabia iliyowauwa watu 143 kisha Pakistan ambayo iliwauwa 135 na Marekani yenye idadi ya watu 42 waliouwawa baada ya kuhumiwa kifo. Nchi hizi tano sinasimamia asilimia 88 ya watu wote waliouwawa mwaka uliopita kutokana na hukumu hiyo.


Idadi ya waliouwawa imeongezeka kutoka mwaka wa 2006 katika nchi za Saudi Arabia, Iran na Pakistan.


Shirika la Amnesty International lenye makao yake mjini London Uingereza limezitaka nchi zinazotumia hukumu ya kifo zihusishe umma wakati wa hukumu hiyo na zisifiche habari zinazohusiana na hukumu hiyo.


Vile vile azimio la Umoja wa Mataifa lililoafikiwa mwaka uliopita na ambalo linazitaka nchi zote zinazotumia hukumu ya kifo ziwache limetajwa katika ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lenye makao yake mjini London Uingereza.