1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani leo zaanza kujadiliana juu ya haki za binaadam

13 Mei 2010

China na Marekani leo zinarejea katika meza ya majadiliano kuhusiana na masuala ya haki za binaadamu, ikiwa ni mara ya kwanza tokea kusitishwa miaka miwili iliyopita

https://p.dw.com/p/NMKk
Rais Barack Obama wa Marekani kushoto akisalimiana na Rais Hu Jintao wa ChinaPicha: AP

Hata hivyo makundi ya wanaharakati wa haki za binaadamu, yanakosoa hatua ya kutoshirikishwa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali katika majadiliano hayo, ambayo watalaam wanayaweka katika mtizamo wa uhusiano wa mataifa mawili yenye nguvu.

Ni miaka miaka miwili sasa tokea majadiliano ya mwisho ya masuala ya haki za binaadamu kati ya mataifa hayo mawili kufanyika.Chanzo cha majadiliano hayo ilikuwa ni uhusiano wa kibiashara kati yao.Mwaka 2000 Umoja wa Mataifa, pamoja na Baraza la Congress la Marekani liliipatia China hadhi ya kibiashara iitwayo Normal Trading NTR ambayo ni hadhi ya kawaida na kuifuta ile ya awali ya kwamba ni taifa linalopendelewa zaidi kibiashara duniani yaani Most Favored Nation MFN.

Hata hivyo sambamba na hadhi hiyo mpya, inategemea pia na ukaguzi wa kila mwaka wa hali ya haki za binaadamu nchini China

Majadiliano hayo ya masuala ya haki za binaadamu yamechukua nafasi ya ukaguzi wa masuala hayo huko China.Lakini swali linalotuama miongoni mwa wanaharakati ni je China baada ya kupewa hadhi hiyo mpya ya kibiashara na Marekani, inahitaji kweli kushughulikia rekodi yake ya masuala ya haki za binaadamu, ili kuendeleza usuhuba wake na Marekani? Mbali na hayo, kumekuwa na shutuma kutoka makundi ya haki za binaadamu kuwa mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili hayawezi kutoa matokeo yoyote mazuri.

Shirika la Amnesty International linashutumu kwa kutoingizwa kwa malengo katika majadiliano hayo.Corinna Barbara Francis kutoka Shirika hilo la Amnesty International anasema kuwa wakati majadiliano hayo yanarejea tena hii leo baada ya kupita kipindi cha miaka miwili, Marekani haitakuwa katika hali kama ambavyo ilikuwa nayo kipindi cha nyuma.

Anasema mabadiliko makubwa katika majadiliano hayo ni kwamba huko nyuma, mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs yalikuwa na mchango mkubwa zaidi katika mjadala, yaliweza kushiriki na kuwasilisha na kuchangia mada.Lakini sasa anasema, mazungumzo yamerejea tena,bila ya kushirikishwa kwa makundi hayo, kwahivyo anaongeza kuwa kwa mtizamo wao, hiyo ni kurudi nyuma kwa hatua kubwa na si kusonga mbele.

Corinna Barbara anasema kuwa mashirika hayo siyo ya kiserikali yana taarifa na takwimu sahihi juu ya yale yanayofanyika katika masuala ya haki za binaadamu na kwamba China imekuwa ikichagiza kutoshirikishwa kwa mashirika hayo.

Muongo mmoja uliyopita umeshuhudia mvutano mkali katika masuala ya haki za binaadamu kati ya Marekani na China.Mwaka 2004 China ilisitisha majadiliano ya awali na haikurejea tena mezani mpaka mwaka 2008, kabla ya kufanyika kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto mjini Beijing.

Hans van Ess profesa wa mafunzo ya kichina katika chuo kikuu cha Ludwig Maximilian mjini Munich hapa Ujerumani anaamini kuwa China ilisitisha kushiriki katika majadiliano hayo mwaka huo wa 2004 kutokana na,vita vya Iraq vilivyoongozwa na Marekani, ambapo Marekani kwa mujibu wa China ilitenda vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Kwa upande wake Corinna Barbara anasema kwa China kuamua kurejea tena katika majadiliano miaka miwili iliyopita, yaani mwaka 2008, ilikuwa ni suala la mahusiano tu kwani ilitaka kuonesha kwamba imepiga hatua katika masuala ya haki za binaadamu, lakini mara baada ya kumalizika kwa michezo ya Olimpiki ikasitisha tena ushiriki wake.

Mazungumzo hayo ya haki za binaadamu kati ya China na Marekani yanayoanza tena hii leo, yalitakiwa kuanza mapema mwaka huu, lakini yalishindwa kutokana na hatua ya Marekani kuiuzia silaha Taiwan.

Hata hivyo Prosefa Van Ess anasema inawezekana kuwa China imeamua kurejea tena mezani katika kipindi hiki, kwasababu ya kufanyika kwa maonesho makubwa ya biashara duniani mjini Shanghai yaliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu.

Katika uhusiano kati ya Marekani na China, wengi wanaona kuwa katika kipindi cha nyuma Marekani imekuwa na tabia ya kubeba jukumu la ukiranja, Lakini hivi sasa China ni taifa kubwa ambalo linabeba kiwango kikubwa cha hati za dhamana za Marekani.Hali hiyo kwa mujibu wa Profesa Van Ess huenda ikaifanya Marekani kubadilika katika majadiliano hayo.

Mwandishi:Sarah Berning

Tafsiri:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman