1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China:Raia wa Kiengereza anyongwa

Miraji Othman29 Desemba 2009

Mtuhumiwa wa madawa ya kulevya anyongwa China

https://p.dw.com/p/LG8H
Mwananchi wa Kichina asoma gazeti mjini ShanghaiPicha: AP

Muingereza Akmal ´Shaikh aliyetuhumiwa kwa ulanguzi wa madawa ya kulevya amenyongwa nchini china mapema leo asubuhi. na huku nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza zikiendelea kukashifu tukio hilo la kuuawa kwa akmal shaikh, wadadisi wa kisiasa wanadokeza kuwa huenda ni ishara ya nchi ya China kuthibitisha msimamo wake wa kujitegemea bila ya muingilio wa nchi zingine zenye ushawishi.peter moss ameandaa taarifa ifuatayo.

Akmal shaikh, mwenye umri wa miaka 53, alikamatwa nchini china akiwa na takriban kilo nne za madawa ya kulevya aina ya heroin katika eneo la Urumqi , kaskazini magharibi mwa china mwaka wa 2007 alipowasili kutoka nchini Tajikistan. Kisa cha shaik ambaye ni baba wa watoto watatu kimegonga vichwa vya habari licha ya jitihada za dharura kutaka asihukumiwe.

Waziri mkuu wa uingereza, Gordon Brown, alisema kwamba ameghadhabishwa na kusikitishwa na mauaji ya shaikh ambaye aliuawa licha ya madai ya kuwa na matatizo ya kiakili. Hata hivyo, viongozi wa mashtaka nchini china walizipuuza tuhuma hizo na kusisitiza kuwa mshtakiwa alikuwa amepatikana na makosa, na hivyo lazima achukuliwe hatua. Akizungumza hapo jana kabla ya kunyongwa kwa Shaikh, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza anayeshughulikia maswala ya jumuiya ya madola, Evan Lewis, alisema kuwa ni hatia kumhukumu mshukiwa ambaye ana matatizo ya kiakili.

´´'Bwana shaikh ni mtu aliyekuwa na matatizo makubwa ya kiakili na sio sawa kwa mtu kama huyo kuuliwa. tumewasiliana mara 27 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ...katika dunia ya sasa sio sahihi kumuua mtu mwenye matatizo ya kiakili´´

Nchi ya China bado inazingatia sera za ukoministi na hukumu ya kifo inatumiwa dhidi ya watu wanaokutikana na hatia ya kuhusika na makosa ya jinai ikiwemo ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Akmal shaikh ni mshukiwa wa kwanza kutoka katika bara la Ulaya kuwahi kuhukumiwa kifo nchini china katika kipindi cha miaka 58. Shirika la kutetea haki za kibinadamu ambalo lina makao makuu jijini London, liitwalo Reprieve,ambalo lilikuwa likimwakilisha mshukiwa kwa kutoa huduma ya kisheria, limetoa taarifa kukashifu sera ya mahakama nchini China na kutaja kuwa ni yenye misingi ya ukandamizaji na yenye kukiuka haki za kibinadamu. Shirika hili la Reprieve lilisisitiza kuwa kupuuzwa kwa hali ya mshukiwa ya kuwa na akili punguani ni kigezo kinachoashiria kuzorota kwa maadili ya ubinadamu.

Akmal Shaikh aliuawa kwa kudungwa sindano yenye sumu.

Duru za marehemu Shaikh zinasema kwamba kupatikana huko kwa madawa ya kulevya huenda kulikuwa njama ya kumhujumu shaikh ambaye hakuwa na historia yoyote ya kuhusika katika visa vya uvunjaji sheria ikiwemo ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Wawakilishi wa Shaikh waliwahi kukata rufaa mara nne kupinga kukamatwa na kuhukumiwa kwa shaikh, juhudi ambazo viongozi wa mahakama nchini china walizitupilia mbali na kusisitiza kuwa kuuawa kwa washukiwa wa madawa ya kulevya ni kigezo kinachozuia visa vya uhalifu na ulanguzi wa madawa haya.

´´kesi hii imeendeshwa kwa mujibu wa sheria za China, kama tunavyofahamu biashara ya madawa ya kulevya ni kosa kubwa sana katika jamii ya kimataifa´´

Familia ya shaikh iliyokuwa imeghadhabishwa na matukio nchini china ilikuwa ikilalamika vikali na kutoa shinikizo kwa china kubatilisha msimamo wake muda mfupi kabla kuuawa kwa shaikh. jamaa na marafiki walikuwa wakikesha na wengine kuchangia katika tovuti iliyoundwa kumtetea Shaikh. Msemaji katika serikali ya china akichangia katika tukio hili alisema anatumai uingereza itazingatia uhalisia wa kesi hii na kutosambaratisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya china na uingereza. shirika hilo la kutete haki za kibinadamu la reprieve linadokeza kuwa washukiwa 1700 wamehukumiwa adhabu ya kunyonwa nchini china tangu mwaka wa 2008

Mwandishi peter moss/ afp

mhariri- Miraji Othman