1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapendeleo au Haki kwa Bernard Tapie?

22 Julai 2016

Mkurugenzi mkuu wa IMF Christine Lagarde atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za uzembe katika kadhia ya fidia ya mamilioni ya Euro alizolipwa tajiri Tapie. Shirika la fedha la kimataifa limeelezea imani yake kwa Lagarde.

https://p.dw.com/p/1JUQ1
Kiongozi wa shirika la fedha la kimataifa IMF Christine LagardePicha: picture-alliance/AP Photo/R. Abd

Korti kuu ya rufaa ya Ufaransa imeyakataa madai ya Lagarde ya kufutiliwa mbali uamuzi wa kumfikisha mahakani kwa dhana za kufanya uzembe katika kuushughulikia ugonvi kati ya benki inayomilikiwa na serikali na mfanyabiashara Bernard Tapie.

Mwaka 2008 Bernard Tapie alilipwa fidia ya Euro milioni 404 baada ya Christine Lagarde kuamuru ugonvi wa muda mrefu kuhusu kuuzwa kampuni kubwa la zana za spoti -Addidas ufumbuliwe kwa njia ya upatanishi.

Uamuzi huo ni pigo kwa mwenyekiti huyo wa IMF ambae daima amekuwa akidai kila alichokifanya amekifanya kwa masilahi ya Ufaransa.

Atakuwa kiongozi wa tatu wa shirika hilo lenye makao yake mjini Washington kufikishwa mahakamani,baada ya Rodrigo Rato wa Uhispania na Dominique Strauss-Kahn wa Ufaransa.

Christine Lagarde alianza kuchunguzwa mwaka 2014 kuhusiana na madai ya jinsi alivyoushughulikia mzozo wa muda mrefu pamoja na Tapie aliyedai ameghilibiwa na benki inayomilikiwa na serikali-Crédit Lyonnais ilipokuwa inaliuza kampuni la Addidas mnamo mwaka 1990.

Kwanini Upatanishi na sio Kortini?

Kesi dhidi ya Lagarde imesababishwa na uamuzi wake wa kuruhusu kesi hiyo ifumbuliwe kwa njia za upatanishi badala ya kupelekwa mahakamani ambako bila ya shaka serikali isingebidi kulipa fidia kubwa kama hiyo.

Frankreich Korruption IWF Christine Lagarde verläßt Untersuchungsrichter
Christine Lagarde akitoka mahakamani Agosti 2014 baada ya kuhojiwa kuhusiana na madai ya rushwaPicha: picture-alliance/dpa

Korti ya sheria ya Ufaransa inahoji upatanishi haukuwa wa haki kwasababu wapatanishi wengi walikuwa wakijuana na Bernard Tapie.

Amri ya korti ya upatanishi ilibatilishwa Februari mwaka jana na korti ya rufaa iliyozungumzia kisa cha udanganyifu na kuthibitishwa pia mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mwaka mmoja jela akikutikana na Hatia

Lagarde amekanusha tuhuma za kufanya makosa yoyote au kupokea amri kutoka kwa rais wa zamani Nicolas Sarkozy ambae Bernard Tapie ni miongoni mwa wafuasi wake wakubwa.

Frankreich Bernard Tapie
Tajiri Bernard Tapie baada ya kuhojiwa na korti ya rufaa Marchi 12 mwaka 2015 mjini ParisPicha: Getty Images/AFP/E. Feferberg

Akikutikana na hatia Christine Lagarde anaweza kuhukimiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na faini ya Euro 15.000.

Wakili wake anaamini kesi hii mpya itamtakasa mwenyekiti huyo wa shirika la fedha la kimataifa aliyekabidhiwa wadhifa huo Julai mwaka 2011 baada ya Strauss-Kahn kulazimika kujizulu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/

Mhariri:Iddi Sessanga