1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Comey kutoa ushahidi dhidi ya Trump

Yusra Buwayhid
8 Juni 2017

Aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI, James Comey, atasimama mbele ya Baraza la Congress Alhamis, kutoa ushahidi dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani unaohusu madao ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka jana.

https://p.dw.com/p/2eIUN
Bildkombo U.S. Präsident Donald Trump und FBI Direktor James Comey
Picha: Reuters/J. Lo Scalzo/G. Cameron

Comey leo atatoa ushahidi wake katika mkutano wa Baraza la Congress unaongojewa kwa hamu kubwa, lakini siku moja kabla alidhihirisha kwamba mara kadhaa Trump alijaribu kuanzisha mazungumzo naye kuhusu uchunguzi wa Shirika la Upelelezi FBI wa madai kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka jana, jambo lililompa wasiwasi mkubwa na kumfanya ajiulize kama rais Trump anajaribu kuingilia uchunguzi huo.

Matokeo ya mkutano wa Comey na Baraza la Congress yatakuwa na athari kubwa kwa utawala wa Trump uliotimiza takriban siku 139, huku mshauri maalumu Robert Mueller pamoja na kamati mbalimbali za Congress zikiwa zinachunguza kama timu ya kampeni za uchaguzi ya Trump ilikuwa na mahusiano na Urusi wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka jana. Ikulu ya Marekani pamoja na Urusi wote wanayakataa madai hayo ya kwamba waliwahi kuwa na uhusiano.

Mwakilishi wa upande wa chama cha Democrat katika Kamati ya Upelelezi ya Baraza la Wawakilishi, Adam Schiff  alizungumza na gazeti la Washington Post Jumatano na kusema uchunguzi wao ndiyo kwanza umeanza.

"Bado tupo katika hatua za awali za uchunguzi, watu lazima wafahamu kwamba FBI ilianza uchunguzi wao tokea Julai mwkaa jana. Sisi tumeanza miezi miwili iliyopita, na hatuna vyanzo vya kufanyia kazi kama vya FBI. Kwahio uchunguzi wetu ndio kwanza umeanza," amesema  Adam Schiff.

Trump alidai kiapo cha utiifu kwa Comey

Katika ushahidi ulioandikwa na kuchapishwa na Baraza la Uchunguzi la Seneti hapo jana, Comey alimnukuu Trump wakati akimwambia kwamba uchunguzi huo unaoihusisha Urusi ni kama wingu linalodhoofisha uwezo wake wa kufanya kazi kama rais wa Marekani. Trump pia alimtaka Comey kukiri hadharani kwamba hayupo chini ya uchunguzi.

USA Michael Flynn in Washington
Aliyekuwa mshauri wa usalama wa taifa kwa Rais wa Marekani, Michael FlynnPicha: Reuters/Y. Gripas

Comey pia amesema Trump alimdai kiapo cha utiifu katika mkutano wao wa Januari 27, siku chache baada ya bilionea huyo wa chama cha Republic kushika wadhifa wa urais  huku akiwa amezungukwa na wingu la madai kwamba Urusi ilimsaidia kushinda katika uchaguzi.

Comey amesema katika ushahidi wake uliochapishwa mapema jana, "Rais aliniambia, 'Mimi ninahitaji uaminifu, Natarajia uaminifu.' Sikuweza kuondoka, kusema, au kubadilisha muonekano usoni mwangu kwa namna yoyote huku kukiwa na ukimya uliyofuata matamshi yake, " aiongeza Comey.

Akiizungumzia kauli hiyo ya Comey juu ya  uaminifu, Seneta wa Republican Richard Burr, mwenyekiti wa jopo hilo linalojumuisha Warebulican na Wademocrat, alijaribu kumtetea Trump kwa kusema: "Sioni kama kuna  makosa ya kuomba uaminifu kutoka mtu yeyote katika utawala wa rais."

Trump alitaka uchunguzi dhidi ya Fynn usitishwe

Comey pia amesema katika taarifa yake hiyo kwamba Febuari 14 alikutana na Trump uso kwa macho katika ofisi ya rais. Comey amesema Trump alimtaka aachane na uchunguzi dhidi ya aliyekuwa mshauri wake wa usalama wa taifa Michael Flynn ambao ni sehemu ya uchunguzi mkubwa zaidi unaoihusisha Urusi.

Wabunge wamesema ushahidi wa Comey utakaosikilizwa leo utazingatia zaidi iwapo Trump alijaribu kupinga haki kutendeka -- mashtaka yaliyomsababisha rais wa zamani wa Marekani Richard Nixon kujiuzulu mwaka 1973.

Trump alianza siku yake kwa kumtangaza mteule wake mpya wa kuongoza shirika la FBI --- Christopher Wray mwanasheria wa uhalifu na aliyekuwa afisa wa Idara ya Sheria wakati wa utawala wa rais George W. Bush. Uteule wa Wray lazima uthibitishwe na Baraza la Seneti.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga