1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CONAKRY : Rais Conte ataka jeshi kuwa kitu kimoja

22 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYz

Rais Lansana Conte wa Guinea anayepigwa vita amelitaka jeshi la nchi yake kuungana kuwa kitu kimoja kukabiliana na mgomo wa taifa ulioidumaza nchi hiyo ambao umegharimu maisha ya watu 10 katika shinikizo la kumtaka an’gatuke.

Umoja wa Afrika umetowa wito wa kufumbuwa kwa njia ya amani mzozo huo uliodumu kwa siku 12 wakati Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS ikitangaza kwamba wapatanishi watakwenda nchini Guinea siku mbili hizi baada ya kuahirisha ziara yao iliopangwa kufanyika hapo jana kutokana na ombi la wananchi wa Guinea.

Conte amekaririwa akisema kwenye televisheni ya taifa hapo jana kwamba wale wanaotaka kuongoza lazima wasubiri zamu yao na kwamba wakati Mungu anapompa mtu madaraka kila mtu hana budi kusimama kidete na mtu huyo.

Conte amelitaka jeshi kuwa kitu kimoja na kutowafuata viongozi wa vyama vya wafanyakazi ambao amesema wamevuka mipaka yao na kujiingiza kwenye siasa.

Conte mwenye umri wa miaka 72 alikuwa na mkutano na viongozi wa kijeshi na wake zao katika Kambi ya Samory katikati ya Guinea hapo Jumamosi.