1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleeza Rice asema Marekani inataka kuona amani mashariki ya kati

15 Oktoba 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza amekutana na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas kujadili mikakati ya kutafuta msimamo wa pamoja kabla ya mkutano wa kilele juu ya suala la amani ya mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/C7he
Picha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice alianza jana ziara yake ya kutia msukumo duru ya mazungumzo ya kidiplomasia ya kutafuta amani katika eneo la mashariki ya kati.Hatua hii inalengo la kuwaleta karibu zaidi waisrael na wapalestina kabla ya kufanyika mkutano wa kilele uliopangwa na Marekani juu ya amani ya eneo hilo.

Hii leo amekutana na kiongozi wa mamláka ya wapalestina Mahmoud Abbas kuzungumzia msimamo wa pamoja kabla ya mkutano huo wa kilele utakaofanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na rais Abbas bibi Rice alisema rais Gorge Bush ameamua kutoa kipaumbele katika suala la kutafuta ufumbuzi wa mzozo kati ya waisraeli na wapalestina.Aidha waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema mkutano wa kimataifa juu ya amani ya mashariki ya kati unaotarajiwa kufanyika Annapolis huko Maryland ni lazima uchukuliwe na umuhimu mkubwa na uhalisi.Na zaidi ya hayo anasema.

‘’Marekani inaona kuundwa kwa dola la Palestina litakalokuwa bega kwa began a Israel ni jambo muhimu kwa mustakabali wa baadae sio tu kwa wapalestina na waisrael bali pia kwa eneo zima la mashariki ya kati na Marekani.’’

Ingawa tayari ilikuwa ikitarajiwa mkutano wa kilele ufanyike Annapolis Marekani Matamshi ya leo ya bibi Rice yamethibitisha rasmi juu ya mahala patakakofanyika mkutano huo.Hata hivyo tarehe na washiriki katika mkutano huo hawajatangazwa.

Hapo jana lakini baada ya duru ya mwanzo ya mazungumzo na viongozi wa Israel maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Mareknai walidokeza kwamba mkutano ulioitishwa na rais Bush kujadili amani ya mashariki ya kati huenda ukakhairishwa sababu kuu ikiwa ni kutofautiana kwa waisrael na wapalestina juu ya ikiwa kuna umuhimu wa kuwa na makubaliano ya mwanzo kabla ya mkutano huo.

Waziri mkuu wa Isreal Ehud Olmert anasema sio muhimu kuwepo sharti la kuweka makubaliano huku rais Abbas akisema kinyume chake,kwamba wapalestina hawatahudhuria mkutano huo bila ya kuwepo makubaliano muhimu yanayogusia masuala yote nyeti ambayo hayajatatuliwa.

Masuala hayo ni pamoja na hatma ya wakimbizi wakipalestina,kugawana Jerusalem, kuwepo mipaka kwa dola la wapalestina na Israel kuondoka ukingo wa Magharibi.

Kwa upande mwingine hii leo rais Mahmoud Abbas amesema anamatarajio kwamba mkutano huo wa kimataifa juu ya mashariki ya kati utaanzisha mazungumzo ya amani yatakayokuwa na mwisho.Halikadhalika aliomba usaidizi wa Marekani katika kuizuia Israel isiendeleze ujenzi wa makazi ya kilowezi pamoja na ukuta wa kujitenga.

Rais huyo wa Palestina pia amezungumzia matumaini yake kwamba wapalestina na waisrel watafikia makubaliano ya kimsingi kabla ya mkutano huo wa kilele.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice pia amepanga kuelekea Misri hapo kesho na kukamilisha ziara yake kwa kufanya mazungumzo nchini Uingereza na mfalme Abdulla wa Jordan mwishoni mwa wiki.