1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleezza Rice arejea Mashariki ya kati.

Mwakideu, Alex31 Machi 2008

Israel yatangaza kujengwa kwa makaazi 1,400 ya wayahudi katika maeneo yanayotarajiwa kumilikiwa na Palestina katika siku za usoni kwa ajili ya ujenzi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/DXzb
Waziri wa nchi za kigeni wa Marekani Condoleezza Rice na Rais wa Palestina Mahmud Abbas wakihutubia wanahabariPicha: AP

Waziri wa nchi za kigeni nchini Marekani Condoleezza Rice yumo katika ziara yake ya pili mashariki ya kazi katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.


Akiwa ziarani katika eneo hilo Rice amesisitiza msimamo wa Marekani wa kupinga ujenzi wa nyumba katika ukanda wa Magharibi ambao Israel inadai ni miliki yake.


Vile vile amekutana na viongozi mbali mbali wanaohusika na mpango wa amani kati ya Israel na Palestina.


Waziri huyo ameanza awamu yake ya pili ya mazungumzo na Rais wa Palestina Mahmud Abbas kama jitahada za Marekani za kurejesha amani Mashariki ya kati.


Rice anatarajiwa kushawishi maendeleo katika mazungumzo hayo ya amani kati ya Rais wa Palestina Mahmud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.


Amewasili leo Amman kutoka Jerusalem ambako alikutana na Olmert siku moja tuu baada ya kushawishi Israel iondoe vzuizi hamsini vya barabarani. Nchi hiyo imeweka mamia ya vizuizi katika barabara za ukanda wa magharibi.


Rice pia amezungumza na mwakilishi wa Palestina katika mpango wa amani ya mashariki ya kati Ahmed Qurei pamoja na waziri wa nchi za nje nchini Israel Tzipi Livni.


Hapo jana Rice alisafiri kutoka Israel hadi Jordan na kukutana na King Abdullah II pamoja na Abbas.


Mazungumzo kati ya Israel na Palestina yalianzishwa tena novemba mwaka uliopita huku pande zote mbili zikiahidi kufikia suluhu mwishoni mwa mwaka huu.


Condoleezza Rice ameelezea furaha yake kuhusu mpango wa amani ya mashariki ya kati akisema kwamba unaendelea vizuri na ana imani Palestina na Israel zitaelewana kabla mwaka huu kumalizika.


Hata hivyo mda mfupi baada ya Rice kuondoka nchini Israel serikali ya nchi hiyo imetangaza kujengwa kwa nyumba 1,400 mpya katika maeneo ambayo Palestina inatajia kuyamiliki katika siku za usoni kwa ajili ya ujenzi wa taila lake.


Wakati huo huo baraza la manispaa la Jerusalem limetangaza mpango wa kujenga nyumba mia sita katika makaazi ya wayahudi katika ukanda wa magharibi.


Tangazo la kujenga makaazi hayo katika maeneo ya Pisgat Zeev limetolewa wakati Rice anafanya ziara ya kujaribu kufanikisha mazungumzo ambayo kulingana na Palestina yanatatizwa na shughli hiyo ya ujenzi wa nyumba inayoendeshwa na Israel.


Hata hivyo msemaji wa waziri mkuu wa Israel amesema hana habari yoyote kuhusu mradi huo wa ujenzi wa nyumba uliopasishwa na manispaa ya Jerusalem.


Mapema waziri mkuu wa Israel Olmert aliambia wabunge wa chama chake cha Kadima kwamba nchi hiyo imeweka wazi nia yake ya kuendeleza ujenzi katika maeneo ya Jerusalem mashariki na ukanda wa magharibi.


Katika miezi ya hivi karibuni Israel imetangaza kujenga mamia ya nyumba kwa ajili ya wayahudi wanaoishi ndani na karibu ya maeneo ya mashariki mwa Jerusalem ambayo nchi hiyo iliyateka pamoja na ukanda wa magharibi wakati wa vita vya mashariki ya kati mwaka wa 1967.


Kwa upande mwengine Rais wa Palestina Mahmud Abbas amesema atakutana na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert aprili tarehe saba. Viongozi hao wawili hawajawahi kukutana kwa wiki saba.


Mkutano wao wa mwisho ulikuwa tarehe tisa mwezi wa pili ambapo Rais wa Palestina aliahirisha mazungumzo kati ya pande hizo mbili kufuatia mashambulizi yaliyokuwa yanatekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza ulioko chini ya utawala wa Hamas.


Mazungumzo ya amani kati ya nchi hizo mbili ha hayajapiga hatua ya maana kwani nchi hizo zimeendelea kutofautiana kuhusu maswala tata yanayozizozanisha na pia zimeendelea kushambuliana katika eneo la ukanda wa Gaza.