1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire ni mshikemshike

Abdu Said Mtullya3 Aprili 2011

Mapigano makali yanaendelea nchini Cote Ivoire baina ya majeshi ya Alassane Ouattara anayetambuliwa na jumuiya kimataifa kuwa rais wa nchi hiyo na yale ya Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madaraka.

https://p.dw.com/p/10maT
Alassane Ouattara akizungumzia kupitia televisheni
Alassane Ouattara akizungumzia kupitia televisheniPicha: AP

Kamati ya kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu imearifu kwamba watu 800 wameuawa mnamo kipindi cha siku moja, kutokana na mapigano hayo.

Hapo awali, majeshi yanayomuunga mkono Gbagbo yaliyarudisha nyuma majeshi yanayomuunga mkono Ouattara, lakini upande wa Ouattara umesema kuwa bado haujaanza kufanya mashambulizi makubwa.

Kapteni Leon Kouakou, ambae ni msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ouattara ameeleza kwamba kwanza majeshi yao yanachukua hatua za kuwadhoofisha maadui zao kabla ya kuanzisha mashambulizi ya kweli.

Hata hivyo, kwa mujibu wa habari, askari wa Gbagbo wamekiteka tena kituo cha televisheni ya serikali, wakati rais huyo wa zamani akiendelea kuipuuza miito inayotolewa na viongozi wa dunia ya kumtaka akabidhi madaraka kwa Ouattara.