1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire.

20 Desemba 2010

Ufaransa na Umoja wa mataifa zimekataa kuondoa vikosi vyao vya jeshi Cote d'Ivoire.

https://p.dw.com/p/Qga3
Wanajsehi wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa mjini AbidjanPicha: picture alliance / dpa

Ufaransa na Umoja wa mataifa  zimelikataa ombi la kiongozi wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo  kuondoa vikosi vyao vya jeshi nchini humo. Umoja wa Mataifa na Ufaransa zimesema kwamba wanajeshi wao watasalia kuwepo Cote d'Ivoire, na wamemshinikiza kiongozi huyo ajiuzulu la sivyo akabiliwe na vikwazo.

Serikali ya Laurent Gbagbo  imezitaka Umoja wa Mataifa na Ufaransa kuviondoa vikosi vyao nchini Cote d 'Ivoire. Katika mahojiano na  vyombo vya habari nchini Ufaransa, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Michele Alliot Marie, amesema kwamba hatua hiyo haitokuwa na maana yoyote kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa, au Ufaransa.

Michele alisisitiza kwamba vikosi hivyo havina nia ya kuhusika moja kwa moja katika vita kati ya wafuasi wa Gbagbo na wale wa mpinzani wake Alassane Outtara, ambao wiki iliyopita walianzisha makabilano ya bunduki.

Hatahivyo waziri huyo amesema kwamba iwapo vikosi hivyo vitashambuliwa moja kwa moja, vina haki ya kujitetea.

Alliot Marie, pia alisisitiza kwamba Gbagbo atakabiliwa na vikwazo vya kimataifa iwapo hatojiuzulu.

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy amesema vikwazo vya Umoja wa Ulaya ikiwemo kupigwa marufuku kusafiri, na kuzuiliwa mali za Gbagbo na wafuasi wake, huenda vitaidhinishwa katika siku zinazokuja.

Laurent Gbagbo analidhibiti jeshi la Cote d`Ivoire na  taasisi kuu za serikali, na kambi yake imekataa wito wa kumtaka kiongozi huyo ajiuzulu ikisema ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi.

Elfenbeinküste Praesident Laurent Gbagbo
Laurent Gbagbo wa Cote d'Ivoire.Picha: Picture-Alliance/dpa

Umoja wa Mataifa,Ufaransa,Marekani,Umoja wa Ulaya, Muungano wa Afrika, na jumuiya ya kibiashara ya mataifa yaliopo magharibi mwa Afrika ECOWAS, wamemuomba  Gbagbo kukubali kushindwa na akubali pendekezo la kwenda uhamishoni.

Hatahivyo msaidizi wa Gbagbo Pascal Affi N'Guessan, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba  hilo ni jambo lisiloweza kufikiriwa na kwamba kila aliyehusika katika mzozo huo, aondoshe fikra kwamba Gbagbo ataondoka.

Kiongozi mpinzani Alassane Outtara amesema kwamba, atakuwa tayari kujadili suluhu, iwapo tu Gbagbo atakubali kujiuzulu.

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Umoja wa mataifa, Navi Pillay amesema kuna ushahidi  wa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu uliotekelezwa na vikosi vya usalama vya Cote D'Ivoire, na amekadiria zaidi ya watu 50 wameuawa katika siku chache  za hivi karibuni.

Mwandishi: Maryam Abdalla/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed