1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Crawford, Texas , Marekani. Bush ashinikizwa kurejesha wanajeshi kutoka Iraq.

25 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWF

Rais George W. Bush, wabunge , wanajeshi wa Marekani na wanasiasa waandamamizi wamekuwa wakitupiana maneno kuhusiana na iwapo nchi hiyo ipunguze idadi ya wanajeshi wake nchini Iraq.

Ikiwa imebaki wiki chache kabla ya ripoti muhimu juu ya maendeleo ya mapambano nchini Iraq hapo Septemba 15, rais Bush anakabiliwa na mbinyo mkali kutangaza kuwa atawarejesha kiasi fulani cha wanajeshi ambao wanafikia 160,000 nchini Iraq.

Ripoti ya awali kutoka katika mashirika 16 ya ujasusi nchini Marekani inaonyesha kuwa viongozi wa kisiasa nchini Iraq hawawezi kutawala lakini imeonya kuwa upunguzaji wa majeshi ya Marekani kunaweza kuongeza ghasia za kimadhehebu.

Wakosoaji kutoka chama cha Democratic wameongeza miito yao ya kumtaka rais Bush kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Iraq, wakati akiwashutumu mahasimu wake hao kisiasa kwa kutaka kuwakatisha tamaa wanajeshi wa nchi hiyo walioko mstari wa mbele nchini Iraq.

Wakati huo huo mwanajeshi mmoja amerejeshwa kutoka Iraq baada ya ndugu zake wawili kuuwawa katika mapambano. Jason Hubbard mwenye umri wa miaka 33 atarejea nyumbani kaskazini ya jimbo la Califonia baada ya mdogo wake Nathan , mwenye umri wa miaka 21 alikuwa mmoja wa wanajeshi 14 kuuwawa katika ajali ya helikopta iliyotokea kaskazini ya Iraq siku ya Jumatano.