1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Croatia yajiunga na Umoja wa ulaya

1 Julai 2013

Maelfu ya wacroatia wamesherehekea kujiunga nchi yao na Umoja wa Ulaya,miaka 22 baada ya kujinyakulia uhuru kutoka Yugoslavia ya zamani.

https://p.dw.com/p/18z1G
Sherehe za kujiunga Croatia na umoja wa ulayaPicha: Reuters

"Karibuni katika Umoja wa Ulaya"Alisema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso mbele ya umati wa watu zaidi ya 20 elfu waliokusanyika mjini Zaghreb muda mfupi kabla ya wimbo wa Umoja wa Ulaya "Utenzi wa furaha" uliotungwa na Beethoven kuhanikiza na bendera za Kroatia na Umoja wa Ulaya kupepea-kitambulisho cha Croatia kuwa mwanachama wa 28 wa Umoja wa ulaya.

"Ni usiku wa kihistoria."Mmeirejesha Croatia katika nafasi yake ya jadi kati kati ya Ulaya-ameongeza kusema Jose Manuel Barroso.

Katika hotuba yake rais Ivo Josipovic wa Croatia amewatolea wito wananchi wenzake wawe na matumaini mema."Tusiachie kiwingu cha mgogoro wa kiuchumi kufunika matumaini yetu.Mgogoro ni changamoto ni wito wa kubuni mustakbal mwema zaidi wa maisha."Amesema rais Ivo Josipovic.

Umoja wa Ulaya kama njia ya kujikwamua kiuchumi

Kroatien wird EU-Mitglied
Bendera za Umoja wa Ulaya(kushoto) na Croatia zapepeaPicha: Reuters

Katika majukwaa matatu yaliyojengwa katika uwanja mkuu wa Zaghreb,zaidi ya wasanii 700,wanamuzi,waimbaji na wachezaji wameonyesha ujuzi wao mbele ya umati wa watu waliojaa furaha. Sherehe kama hizo zimefanyika pia katika miji ya Split na Dubrovnik,sawa na Varardin na Riejka.

Marais wa nchi zote za Balkan walihudhuria sherehe hizo mjini Zaghreb sawa na mamia ya viongozi wa kimataifa.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani sawa na waziri mkuu wa Uingereza na rais wa Ufaransa hawakuhudhuria sherehe hizo.

Croatia inafuatia Rumania na Bulgaria zilizojiunga na Umoja wa ulaya tangu mwaka 2007.Uchumi wa Croatia unadorora tangu mwaka 2009 na ukosefu wa ajira unafikia asili mia 20 ya wakaazi milioni 4 na laki mbili.

Serikali ya kati kushoto inategemea kwa kujiunga na Umoja wa ulaya,wawekezaji wa kigeni watapata moyo na kusaidia kuinua shughuli za kiuchumi.Pato la ndani la kila mkaazi linagonga asili mia 39 chini ya pato la wastani katika nchi za Umoja wa ulaya,pekee Rumania na Bulgaria ziko nyuma ya Kroatia-kwa mujibu wa idara ya takwimu ya Umoja wa Ulaya.

Walala hoyi laki tatu"nanai atasherehekea?Ndo kusema Umoja wa ulaya una dawa ya matatizo hayo?Amejiuliza mwana mtandao mmoja kupitia mtandao wa kijamii Facebook.

Croatia ni ya pili baada ya Slovenia kujiunga na Umoja wa Ulaya baada ya kuvunjika shirikisho la jamhuri za zamani za Yugoslavia katika miaka ya 90.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu