1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CSU na Matatizo ya kujitakia Magazetini

Oumilkheir Hamidou
17 Septemba 2018

Mkutano mkuu wa chama cha CSU mjini Munich, uhusiano kati ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD na kile kinachoeneza chuki dhidi ya waislam Pegida na mashindano ya mbio za nyika mjini Berlin magazetini.

https://p.dw.com/p/34z9q
Deutschland CSU Parteitag in München
Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Kusini mwa Ujerumani mjini Munich kulifanyika mkutano mkuu wa chama cha jimbo hilo, CSU, ambao ulitoa sura ya mshikamano miongoni mwa wanachama wake, wiki nne tu kabla ya uchaguzi unaoashiria uwezekano wa chama hicho kupoteza wingi wa viti bungeni.

Vyama vyengine, na hasa kile cha Social Democrat, vinaweza kuchukulia kama mfano wa kuigiza: chama cha CSU kinazongwa na mzozo mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu miaka ya 50. Kinafanya nini badala yake? Linahoji gazeti la Schwäbische Zeitung.

Mhariri anasema kuwa CSU kinasherehekea na kujitaja kuwa mhimili wa utulivu kwa jimbo hilo huru la kusini. Na wote wakashikana mikono jukwaani, hata wale ambao hadi wakati huu hawakuwa wakishirikiana, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa chama Horst Seehofer na waziri mkuu Markus Söder.

Tofauti kati ya AfD na Pegida iko wapi?

Mshikamano huo wa nguvu uliweza kuficha sura halisi ya chama cha CSU kinachokabwa na matatizo ya kila aina wiki nne kabla ya uchaguzi wa jimbo. Kibaya zaidi kwa Söder, Seehofer na wengineo ni kwamba matatizo yote hayo wamejitakia wenyewe. Wiki zinazokuja, CSU hakitafanikiwa kushughulikia vyanzo vya matatizo yake. Kilichobakia sasa ni "kufunika kombe" na baada ya Oktoba 14, chama cha CSU kitabidi kitafakari na kujiuliza mipaka ya matatizo inaishia wapi?

Maandamano yaliyotokea Chemnitz na Köthen yametoa picha ya mshikamano wa aina fulani uliopo kati ya wafuasi wa chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani (AfD) na wale wa chama kinachowapinga Waislamu, Pegida. Gazeti la "Sächsische Zeitung" la mjini Dresden linachambua uhusiano uliopo kati ya makundi hayo mawili na kuandika kuwa mkutano huo mkuu wa chama cha AfD tawi la Sachsen umeamua kusiweko na mshikamano pamoja na Pegida.

Lakini hilo limeshatokea. Kwamba AfD na Pegida hawana tofauti katika malengo yao na matamshi yao, kila mmoja analiona na kulisikia. Pekee viongozi wachama hicho mjini Berlin ndio wanaojidai hawautambui ukweli huo.Tafiti zote za maoni ya wananchi zinaonyesha wale wanaowapigia kura AfD hawawapigii kwasababu ya suala la maadili au hishma. Anaewapigia kura wafuasi wa siasa kali za kizalendo anapiga kura tu, hazingatii lolote. Na hilo linamaanisha pia mbinu zozote dhidi ya chama kama hicho huishia  mara zote kuwapa nguvu.

Mbio za nyika na rekodi zake

Mada yetu ya mwisho magazetini inatuteremsha viwanjani. Katika mbio za nyika zilizofanyika Berlin jana, Eliud Kipchoge wa Kenya ameivunja rekodi ya dunia iliyowekwa na mkenya mwenzake Dennis Kimetto mwaka 2014 kwa zaidi ya dakika moja. Amezunguka masafa ya kilomita 42.195 kwa saa mbili dakika moja na sekondi 39. Gazeti la Badische Neuste Nachrichten  linaandika:

Katika mashindano ya mbio mfano wa Berlin na jumapili inayokuja Karlsruhe, kuna washindi wanaoweka muda bora tu. Katika mashindano kama hayo rikodi daima zinavunjwa na wale ambao mwishoe hakuna anaewataja: Watu wengi wanaoshiriki katika mashindano hayo ya kilomita 42.195 au yale ya kilomita 21.1 wanajitahidi wawezevyo kuweka muda bora kwao wao wenyewe. Hata kama muda huo unakuwa nyuma kwa saa moja au mbili na ule wa rikodi ya dunia.

 

Mwandishi: Hamidu Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef