1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba yajitayarisha kwa kipindi cha maombolezi

Sekione Kitojo
27 Novemba 2016

Wacuba wanajitayarisha na kipindi rasmi cha maombolezi, baada ya kifo cha rais wa zamani na kiongozi wa mapinduzi Fidel Castro. Mdogo wake, Raul, amesema mwili  wa Fidel utachomwa moto kwa utashi wa kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/2TJdE
Fidel Castro
Kiongozi wa zamani wa Cuba , rais Fidel CastroPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Majivu  ya  Castro  watazikwa  katika  mji  wa  Santiago de Cuba baada  ya  siku  nane za maombolezi  rasmi ya  kitaifa, ambayo yanatarajiwa  kufikia  mwisho Desemba  4.

Umma  utaruhusiwa  kushuhudia  mwili  wa  Castro Jumatatu  na Jumanne , katika  eneo  la  makumbusho  la  Jose Marti  mjini Havana , na  kisha  kutakuwa  na  sala  maalum  ya  kumuaga  siku ya  Jumanne  katika  uwanja  mkuu  wa  mapinduzi  mjini  humo.

Gwaride  nchi  nzima  litafuatia katika  muda  wa  siku  nne, kwa matembezi  ya  jumla  ya  kilometa  900 kutoka  mji  mkuu   wa  Cuba Santiago, na  mkutano  mkubwa  wa  pili  wa  sala  utafanyika  siku ya  Jumamosi.

Fidel Castro in Berlin
Fidel Castro akiwa wakati alipofanya ziara Berlin Mashariki katika iliyokuwa Ujerumani masharikiPicha: picture-alliance/AP Photo/R. More

Maafisa  wa  Cuba  wamesema  tukio  la  mazishi  linatarajiwa kufanyika  katika  makaburi  ya  Santa Ifigenia  mjini  Santiago Desemba  4.

Mshairi  na  mwanasiasa  wa  jamhuri  Jose Marti  pia  amezikwa hapo. Katika  kipindi  cha  maombolezi  hakutakuwa  na  shughuli ama  matamasha  ya  wazi , bendera  zitapepea  nusu  mlingoti katika  majengo  ya  serikali  na  radio  na  televisheni  zitatangaza vipindi  vya  taarifa, uzalendo  na  historia, maafisa  wamesema.

Kuba Fidel Castro Rede auf dem Platz der Revolution 1965
Castro akihutubia katika uwanja wa Mapinduzi mjini HavanaPicha: Getty Images/Keystone

Picha  za  hivi  karibuni  zilizochapishwa  za  Fidel Castro  zilikuwa za  Novemba  15, wakati  alipokutana  na  rais  wa  Vietnam  Tran Dai Quang. Tukio  lake  la  mwisho  kuonekana  hadharani  lilikuwa Agosti 13  katika  ukumbi  wa  matamasha  wa  Karl Max  mjini Havana. Tangu  kuondoka  madarakani  mwaka  2006, Fidel Castro alijing'atua  kutoka  katika  siasa  halisi.

Kifo  cha  Castro  usiku  wa  Ijumaa  akiwa  na  umri  wa  miaka  90 kilitangazwa  katika  televisheni  ya  taifa  na  mdogo  wake  wa kiume  Raul Castro. Afya  ya  Castro  iliwekwa  siri  kwa  kiasi kikubwa  nchini  Cuba. Hakuna  taarifa  iliyotolewa  kuhusiana  na sababu  za  kifo  chake.

Mahasimu wafurahia kifo cha  Castro

Wakati  huo  huo  Wamarekani  Wacuba  walimiminika  mitaani  mjini Miami  siku  ya  Jumamosi (26.11.2016) wakiimba "Cuba Libre!"  na "Uhuru ! Uhuru !"  wakati  wakisherehekea  kifo cha  adui yao mkubwa Fidel Castro.

Kubanischer Revolutionsführer Fidel Castro gestorben
Karatasi pamoja na maua yaliyowekwa kumshukuru Castro kwa yote aliyowatendea Wacuba baada ya kifo chake . "Asante Fidel "Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Watu  hao  waliokuwa  wakisherehekea , wengi  wao  waliukimbia utawala  wa  kikomunist   wa  Havana  walipiga   honi, kupiga  sufuria na  ngoma , na  kucheza, wakilia , na  kupeperusha  bendera  ya Cuba  katika  hali  ya furaha  kubwa  katika  jamii  hiyo.

Mjini  Miami , ambako  wanaishi  Wamarekani  Wacuba  wengi nchini  Marekani,  taarifa  hizo  zilisambaa  haraka kwa hamasa. "Ni masikitiko  kwamba  mtu anafurahia  kifo  cha  mtu  mwingine , lakini mtu  huyu  hakupaswa  kuzaliwa," alisema  Pablo Arencibia , mwenye umri  wa  miaka  67, mwalimu ambaye  alikimbia  kutoka  Cuba miaka  20  iliyopita.

USA Exil-Kubaner jubeln nachdem Fidel Catro gestorben ist
Wacuba wanaoishi uhamishoni Miami nchini Marekani wakisherehekea kifo cha CastroPicha: picture alliance/dpa/G. De Cardenas

Wakitanabahi  kuhusu  tukio  la  kihistoria , vijana  waliokuwa wakifurahia  waliweka  tukio  hilo moja  kwa  moja  katika  ukurasa wa  Facebook, waliweka  picha  katika  ukurasa  wa Instagram, na walionesha  sherehe hizo  katika  Face Time  na  Skype  kwa marafiki  na  ndugu  katika  kisiwa  hicho.

Havana  ndogo  na  Hialeah , maeneo  ambako  Wacuba  wengi wanaoishi  uhamishoni  wanaishi , waliona  watu  wakicheza, kukumbatiana  , na  kuzungumza, kwa  kusema "ilichukua  muda mrefu  sana ," na  "sasa ni  zamu  ya  Raul."

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Mwehozi, Sylvia