1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Tanzania bado wanaishi katika umasikini

Amina Mjahid
14 Aprili 2021

Chama cha upinzani Tanzania CUF kimesema licha ya taifa hilo kutangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati lakini bado idadi kubwa ya wananchi, wanaishi chini ya mstari wa umasikini, hii ikichangiwa na ukosefu wa ajira

https://p.dw.com/p/3rz9E
Tansania Dar es Salaam | Partei CUF | Ibrahim Lipumba
Picha: DW/S. Khamis

Kingine kilichochangia uwepo wa umasiki kwa wananchi wa Tanzania ni uvunjiifu wa hakina hata kufanya miradi ambayo hainufaishi idadi kubwa ya wakaazi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Hayo ni sehemu ya maazimio ya baraza kuu la chama hicho cha upinzani ambacho kiliwahi kuwa sehemu ya dola kwa upande wa Zanzibar, baada ya kuhitimisha mkutano wake uliopokea taarifa mbalimbali, ikiwemo misiba ya kitaifa na hali ya uchumi inayoendelea Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya baraza hilo, mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba amesema, licha ya taifa kuingia katika uchumi wa kati kwa kiwango cha chini kitakwimu, bado idadi kubwa ya wananchi hasa waliopo mijini wanaishi katika lindi la umasikini, hali ambayo imechochewa zaidi wakati wa mripuko wa janga la virusi vya Corona.

Akitumia takwimu za Benki ya Dunia, Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi wa kimataifa, amesema katika mwaka 2020, zaidi ya Watanzania laki sita waliingia katika lindi la umasikini, huku zaidi ya wengine milioni 28 wakitopea kwenye umasikini, hali ambayo inawafanya watu wa taifa hili kubwa kabisa la Afrika Mashariki lenye idadi kubwa ya maliasili yakiwemo madini mbalimbali, kutokuwa na furaha kwa mujibu wa rikodi za kidunia.

"Kwa kutumia kigezo cha umasikini cha taifa, idadi ya watanzania maskini imeongezeka kutoka asilimia 26.1 mwaka  2019 na kufikia asilimia 27.2 mwaka 2020 na watanzania zaidi ya milioni 15 ni masikini," alisema Lipumba.

CUF: Milango iko wazi kwa wanachama waliohama kurejea ili kukistawisha chama

Ringen um neue Verfassung in Tansania
Mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania CUF Profesa Ibrahim Lipumba Picha: DW/M.Khelef

Akizungumzia hoja ya kukijenga chama hicho ambacho kiliingia katika mgogoro wa ndani uliosababisha  maelfu ya wanachama kuhamia vyama vingine wakiongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, mwenyekiti huyo wa CUF amebainisha kuwa baraza kuu la chama chake limeweka milango wazi kwa wanachama waliohama kurejea kundini ili kukistawisha chama hicho kilichowahi wakati fulani kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Itakumbukwa kuwa CUF iliweka wazi msimamo wake wa kutoshiriki mchakato wowote wa kidemokrasia hadi pale katiba mpya iliopendekezwa na wananchi itakapopitishwa kutokana na kile walichokitaja kubakwa kwa demokrasia katika uchaguzi mkuu 2020. Lakini sasa Profesa Lipumba anasema wanatathmini mwenendo wa siasa chini ya Rais Samia Suluhu na huenda maamuzi yakawa tofauti.

"Kamati ya uongozi wa ya taifa iendelee kutathmini hali ya kisiasa ya nchi chini ya rais mpya kwahiyo msimamo wetu utategemea kama kuna mabadiliko chanya," aliongoza kusema Lipumba

Msimamo kama huu wa CUF unaonekana kuwa wa vyama vingine vya upinzani vilivyotangaza kuhujumiwa katika uchaguzi mkuu wa 2020, ambavyo navyo vinatazama muelekeo wa kisiasa chini ya rais wa sita na wa kwanza mwanamke, Samia Suluhu Hassan, kutokana na mwanzo wake kuonekana kutaka maridhiano ya kitaifa.

Mwandishi: Hawa Bihoga/Dw Dar es salaam