1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CUF: Serikali ya Tanzania ianze maandalizi ya Sensa

27 Aprili 2021

Chama cha upinzani nchini Tanzania CUF kimeitaka serikali nchini humo, kuanza maandalizi ya sensa ya watu na makaazi, ili kutoa nafasi kwa shughuli hiyo kufanyika kwa ufanisi.

https://p.dw.com/p/3sdHn

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa chama hicho profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema, licha ya utaratibu ambao nchi imejiwekea wa kufanya sensa ya watu na makazi kwa kila baada ya kipindi cha miaka kumi, ikiwa imebaki takriban mwaka mmoja na miezi kadhaa hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ambayo yanaonekana kufanywa na serikali na wadau wake.

Amesema katika sensa ya mwaka 2012 kulikuwa na mapungufu kadhaa ambayo yalitokana na serikali kutojiandaa vema hatua iliosababisha baadhi ya watu kususia zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa kwenye matokeo ya kutohesabiwa, hivyo kuitaka serikali inayoongozwa na Rais Samia Hassan Suluhu kuhakikisha inajiandaa mapema ili kulifanya zoezi hilo kikamilifu.

Aidha chama hicho cha upinzani kikilitazama suala la demokrasia kwa mapana yake ambayo ilionekana kuzorota zaidi katika awamu iliopita.

CUF imesema inaridhika kuwa serikali ya awamu hii imejipanga katika kurejesha mahusiano na mashirikiano na mataifa mengine kadhalika na taasisi za kidunia ambazo zililitazama taifa hilo kama si sehemu ya uhakika ya kuwekeza kutokana na kutotabirika kwa sera zake za kikodi pamoja na matamko ya kisiasa yalioleta athari kwa wawekezaji.

CUF yasema utawala mpya unatia moyo

Tansania Anhänger der Oppositionspartei (CUF) während der Veranstaltung zur Begrüßung ihres Vorsitzenden Prof. Ibrahim Lipumba
Picha: DW/S. Khamis

Itakumbukwa kuwa katika awamu ya uongozi iliopita kulishuhudiwa baadhi ya watanzania wakipoteza ajira zao kutoka na sekta ya uwekezaji kuzorota nchini humo huku baadhi ya wawekezaji wakiondosha biashara zao kutokana na kodi kubwa,.

Masuala mengine yalikuwa matamshi ya kisiasa ambayo yalizorotesha sekta hiyo ambayo ilitoa ajira kwa idadi kubwa ya wananchi ambao wengi kati yao wanaishi chini ya dola mbili na nusu.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho wameiambia DW kuwa, katika suala la democrasia ya vyama vingi, wanaona mwangaza mpya baada ya kuminywa kwa takriban miaka mitano iliopita, hivyo kuwataka viongozi wa kisiasa ambao watakutana na Rais Samia mbali na kuzungumzia suala la katiba mpya wazitazame upya sheria zote ambayo zimepora uhuru wa democrasia ikiwemo sheria ya vyama vya siasa.

Hata hivyo matarajio ya wafuatiliaji wa mambo wanasema dhamira ya Rais Samia kukutana na vyama vya siasa itakamilika muda mfupi baada ya kukabidjhiwa uwenyekiti na chama chake CCM na kuipanga safu ya uongozi akiwemo katibu mkuu wa chama hicho, ili kuleta uwakilishi sawa wa vyama vya siasa.