1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DARFUR: Mkutano wamalizika bila kufikia muafaka

23 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBNR

Umoja wa mataifa na umoja wa nchi za Afrika zimeshindwa kufikia muafaka juu ya uraia wa askari 26,000 wanaotarajiwa kuunda kikosi cha kulinda amani kitakacho pelekwa katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Sudan inasisitiza kwamba imekubali kupelekwa askari wa kulinda amani katika jimbo la Darfur kwa sharti kuwa kikosi hicho kiwe cha askari wa Umoja wa Afrika lakini umoja wa mataifa umesema kwamba ijapokuwa nchi kadhaa za Afrika zimekubali kuchangia askari hao lakini sio zote zinazotimiza kiwango cha umoja wa mataifa.

Licha ya mkutano huo kumalizika bila ya kufikia muafaka katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amesema kwamba mkutano huo ulikuwa wa muhimu na kwamba juhudi zitaendelezwa ili kufikia mafanikio katika mikutano ya baadae itakayo jadili maswala ya kisiasa.

Kiongozi wa kundi la waasi ambae ana ushawishi mkubwa amependekeza kwamba ni bora kuwa na idadi kubwa ya askari wa kigeni kuliko askari kutoka umoja wa Afrika katika kikosi hicho na ametishia kususia mazungumzo ya amani ya mwezi ujao yatakayofanyika nchini Libya.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Negroponte ameonya kwamba kiongozi yoyote wa kundi la waasi atakae susia mazungumzo ya amani ya tarehe 27 mwezi Oktoba mjini Tripoli, Libya atakabiliwa na hatua kali.