1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DCI wa Kenya athibitisha sauti iliyovuja ni ya Wetangula

Grace Kabogo
22 Mei 2019

Sakata la dhahabu bandia limechukua mwelekeo mpya baada ya idara ya ujasusi ya Kenya kumtaka Seneta wa Bungoma Moses Wetangula kujibu maswali atakaporejea kutoka China huku ikithibitisha kuwa sauti iliyovuja ni yake.

https://p.dw.com/p/3Iry7
Flagge von Kenia
Picha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE umejisogeza mbali na kashfa hiyo na kuweka bayana kuwa ni biashara ya binafsi wala sio ya kati ya mataifa.

Kwa mara ya kwanza tangu kashfa ya dhahabu bandia kugonga vichwa vya habari, balozi wa Umoja wa Falme za kiarabu, UAE nchini Kenya, Khalid Al Mualla amejisogeza kando na kadhia hiyo. Balozi Khalid Al Mualla aliyezungumza na gazeti la Daily Nation alisisitiza kuwa makubaliano hayo ya biashara yalikuwa ya binafsi wala sio rasmi kati ya Kenya na Dubai.

Kadhalika ameweka bayana kuwa Ali Zandi aliyeripotiwa kuwa jamaa wa mwanamfalme Sheikh al-Maktoum kiongozi emir wa Dubai si raia wa UAE kwa hiyo hawezi kuwa mpwa wake. Hata hivyo hakufafanua iwapo anahusika na biashara ya kuagiza dhahabu kutokea Kenya hadi Dubai.

Kuhusu waraka wa malalamishi, balozi huyo alisisitiza kuwa hakuna barua yoyote iliyowasilishwa kwani yeye ndiye angekuwa mshenga na hajalifanya hilo. Ifahamike kuwa maafisa wa ujasusi wa Kenya wako Dubai kumhoji Ali Zandi ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya dhahabu ya Zlivia.

Kenia Mombasa - Hassan Ali Joho (kenianischer Politiker)
Gavana wa ODM Mombasa, Ali Hassan JohoPicha: Jacob Safari

Kwa hapa nchini kampuni ya Zlivia inamshirikisha Zahir Jhandi ambaye ni mfanyabiashara anayesisitiza kuwa hajawahi kuuza dhahabu ila ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo. Hadi sasa hakuna mlalamikaji rasmi, suali ambalo yeye Zahir Jhandi nalo pia analiuliza.

Itakumbukwa kuwa Zahir Jhandi aliwahi kuwania ubunge wa eneo la Nyaribari Cache na anatokea Kisii. Yote hayo yakiendelea, mkuu wa idara ya ujasusi nchini Kenya, DCI, James Kinoti amethibitisha kuwa sauti iliyovuja mtandaoni mwishoni mwa juma lililopita kwenye mawasiliano ya biashara ya dhahabu ni ya Seneta wa Bungoma Moses Wetangula. Tamko hilo linatolewa baada ya idara hiyo kuamuru waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, ahojiwe na kujibu maswali pindi atakapowasili nchini. 

Kwa sasa Wetangula yuko China anakohudhuria kongamano la kupambana na ufisadi na mpaka sasa hajatoa kauli yoyote. Hapa nyumbani, viongozi wa chama cha upinzani cha ODM wanaendelea kumtetea kinara wao Raila Odinga ambaye ametajwa kuhusika na sakata hiyo. Gavana wa ODM wa Mombasa Ali Hassan Joho anashikilia kuwa mafisadi wanajulikana.

Kwa upande wake Seneta wa Siaya James Orengo amemtolea wito Mwendesha mashtaka mkuu Noordin Haji kuiongeza kasi ya uchunguzi na kuwafichua waliohusika na kashfa hiyo ya dhahabu bandia. Inasadikika kuwa kiongozi wa Dubai alipoteza kiasi cha shilingi milioni 400 kwenye mpango wa dhahabu ambayo hadi sasa haijulikani iliko.