1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dedan Kimathi, shujaa wa ukombozi wa Kenya

12 Desemba 2013

Dedan Kimathi, kiongozi wa kundi la Mau Mau lilipombana kwa silaha dhidi ya ukoloni wa Uingereza, na ambaye tawala zilizopita nchini humo zilikataa kumpa heshima yake, anaangaliwa sasa kama shujaa wa ukombozi.

https://p.dw.com/p/1AXj4
Sanamu ya Dedan Kimathi jijini Nairobi iliyowekwa mwaka 2006 kutambua mchango wake kwenye harakati za ukombozi.
Sanamu ya Dedan Kimathi jijini Nairobi iliyowekwa mwaka 2006 kutambua mchango wake kwenye harakati za ukombozi.

Awamu mbili za utawala wa mwanzo wa Kenya baada ya uhuru, ile ya Mzee Jomo Kenyatta na baadaye wa mrithi wake, Daniel arap Moi, zilikataa kumtambua na kumpa Kimathi heshima ya kuwa mpiganiaji uhuru, zikimuangalia kama gaidi.

Lakini baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na kuingia madarakani kwa Rais Mwai Kibaki hapo mwaka 2006, serikali ilimtangaza Kimathi kuwa ni shujaa wa vita.

Dedan Kimathi Waciuri aliyezaliwa akipewa jina la Kimathi wa Waciuri tarehe 31 Oktoba 1920, alikuwa kiongozi wa kundi la mau mau lililokamata silaha katika kile kilichojulikana kama uasi wa Mau Mau dhidi ya ukoloni wa Uingereza nchini Kenya mnamo miaka ya 1950.

Kimathi alizaliwa huko Thegenge kijiji cha eneo la Tetu katika Wilaya ya Nyeri. Baba yake mzazi alikuwa na wake watatu, lakini alifariki dunia kabla ya Kimathi kuzaliwa. Kimathi alilelewa na mama yake, Waibuthi. Alikuwa na ndugu wawili wa kiume, Wambararia na Wagura, na dada zake wawili.

Alipofika umri wa miaka 15, alijiunga na shule ya msingi kijijini kwao, Karuna-ini, ambako alijifunza Kiingereza kwa ufasaha na kuitumia lugha hiyo baadaye kuandika mengi kabla na baada ya uasi wa Mau Mau. Alikuwa mtu aliyeshiriki sana katika mijadala shuleni na alikuwa na kipaji cha kuandika mashairi.

Harakati za Mau Mau

Rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta.
Rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta.Picha: AP

Mwaka 1940, Kimathi alijiunga na jeshi la Uingereza lakini akaachishwa mwezi mmoja tu baadaye kwa kosa la ulevi na kupigana na kuruti wenzake. Baadaye alifanya kazi moja baada ya nyengine, ikiwa ni pamoja na kuchunga nguruwe na mwalimu wa shule ya msingi ambako nako alifukuzwa kutokana na madai ya kutumia nguvu dhidi ya wanafunzi wake.

Kati ya mwaka 1947 na 1948 wakati akifanya kazi huko Ol Kalou, Kimathi alikutana na wanachama wa Kenya African Union (KAU) na ilipofika 1950 akachaguliwa katibu wa tawi la chama hicho cha KAU katika eneo la Ol kalou, lililokuwa likidhibitiwa na wafuasi wa mapambano ya Mau Mau.

Mau Mau ilianza kama la Wakikuyu waliodai ardhi walionyang'anywa na walowezi wa Kiingereza. Wakati ushawishi na ukubwa wa wanachama ukitanuka, kundi hilo likawa kitisho kikubwa kwa wakoloni.

Baada ya kula kiapo cha Mau Mau mwaka 1951, Kimathi alijiunga na tawi la kijeshi la chama kilichovunjika cha Kenya Central Association.

Akiwa katibu mkuu wa tawi, Kimathi alisimamia hafla za wanachama kula kiapo na aliamini katika kuwalazimisha Wakikuyu wenzake kula kiapo cha mshikamano na vuguvugu la kupigania uhuru. Alitumia hata njia za kupiga na vitisho kwa kutumia bastola kulazimisha hilo lifanyike.

Kimathi alikamatwa kwa muda mfupi lakini akaachiwa kutoroka mwaka huo huo kwa msaada wa polisi na huo ukawa mwanzo wa uasi dhidi ya wakoloni. Mwaka 1953, Kimathi akaunda Baraza la Ulinzi kuratibu shughuli za wapiganaji wote wa msituni.

Kukamatwa na kunyongwa

Mwaka 1958, miaka minne tangu kuanza uasi huo, Kimathi alikamatwa katika misitu ya Nyeri na kundi lililoongozwa na Ian Henderson. Kukamatwa kwake kukawa mwisho wa vita vya msituni.

Alihukumiwa kifo na Jaji Mkuu O`Connor katika mahakama ambayo jopo zima lilikuwa la Wakenya weusi, huku akiwa kitandani hospitali kuu mjini Nyeri. Alinyongwa mapema asubuhi ya tarehe 16 Februari 18 1957 katika gereza kuu la Kimiti

Mahala alipozikwa hadi leo hapajulikani. Kimathi anaangaliwa kama shujaa wa taifa na serikali ya sasa na kuna sanamu maalum la "Mpigania Uhuru Dedan Kimathi" katikati ya jiji la Nairobi, lililozinduliwa tarehe 11 Desemba 2006, katika kumbukumbu ya tarehe aliyouwawa.

Kimathi alimuowa Mukami Kimathi. Miongoni mwa watoto wao kuna wanaume, Wachiuri na Maina na wanawake, Nyawira na Wanjugu. Mwaka 2010 mkewe Kimathi aliomba msako wa kutafuta mwili wa hayati mumewe uanze tena ili aweze kumzika kwa heshima.

Imetafsiriwa na Mohammed Abdul-Rahman
Chanzo: Wikipedia
Mhariri: Mohammed Khelef