1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Goldberg apewa heshima

Abdu Said Mtullya26 Aprili 2013

Kurasa za historia ya Afrika Kusini haziwezi kujaa bila ya jina la Denis Goldberg. Ni mwanaharakati mashuhuri aliepambana na utawala wa kibaguzi nchini Afrika kusini. Jee yeye ni nani hasa?

https://p.dw.com/p/18NSc
Nelson Mandela na Goldberg
Nelson Mandela na Dennis GoldbergPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya kuishi katika kitongoji cha walala vyema, Goldberg, ambae ni mtoto wa mhamiaji wa kiyahudi ameendelea kuwa Mkomunisti. Na bado ni shabiki wa Rais Jacob Zuma. Mwanaharakati huyo wa mapambano ya kitabaka anatimiza umri wa miaka 80 mnamo mwezi huu. Na kwa ajili hiyo Wakfu wa mazingira na maendeleo wa jimbo la Ujerumani la Northrhine Westphalia unamuenzi mpigania uhuru huyo.

Mwelekeo wa maisha ya Goldberg ulibadilika kabisa alipotimiza umri wa miaka 30. Alipatikana na hatia ya uhaini na hujuma kwenye kesi maarufu ya Rivonia mnamo mwaka wa 1964. Mahakama ya makaburu ilimtia hatiani yeye pamoja na Mandela na wapigania uhuru wengine 15.

Kutokana na shinikizo la familia yake Goldberg alisomea uhandisi wa ujenzi. Kutokana na msimamo wake wa kutetea haki, Goldberg alijiunga na Wakomunisti na chama cha African National Congress ambacho sasa kinatawala nchini Afrika Kusini. Goldberg ni mdhanifu mwenye malengo, pia ni mwanaharakati wa mapambano ya kitabaka mpaka leo licha ya kuishi katika kitongoji cha walala vyema cha Hout Bay:

Mfumo wa kibepari

Goldberg amesema kwamba tathmini juu ya ubepari iliyomo katika mafunzo ya Marx na Ukomunisti bado haijabadilika mpaka leo. Ni kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita. "Naishuhudia dunia ya uroho inayoimeza pia Afrika Kusini." Goldberg amesema uroho huo unaiteketeza nchi kwa sababu haupunguzi umasikini bali unauzidisha. Na hilo siyo jambo la sadfa. Huo ndio msingi wa kampuni. Bila ya kujali iwapo zinaongozwa na za Wazungu au Waafrika."

Tokea mwanzoni mwa miaka ya 60 baada ya chama cha ANC, chini ya Mandela kubalidilisha mkakati wa harakati za kupigania uhuru,na kuanza kutumia mtutu wa bunduki badala ya kampeni za kisiasa,Goldberg tayari alikuwapo.

Akamatwa na kufungwa:

Ustadi wake katika uhandisi ulikuwa muhimu kwa tawi la kijeshi la ANC-Umkhoto we Sizwe.Goldberg alikuwa mshauri wa mambo ya kifundi wa tawi hilo.Mnamo mwaka wa1963 alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miasha jela mara nne.Lakini tofauti na Mandela ,Goldberg alifungwa kwenye jela ya weupe ya mjini Pretoria,badala ya kupelekwa kwenye kisiwa cha Robben.

Goldberg aliitumia fursa ya jela kufanya masomo kwa njia ya posta. Alipofunguliwa mnamo mwaka1985 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 22, Goldberg ambae wakati huo alikuwa na umri wa miaka 52 aliamua kwenda kwa mkewe mjini London. Goldberg pia alikiwakilisha chama cha ANC kwenye Umoja wa Mataifa.

Arejea Afrika Kusini:

Mwanaharakati huyo alirejea nchini Afrika Kusini mnamo mwaka wa 2002 baada ya kufanyika uchaguzi wa kwanza huru. Wakati huo pia mkewe alifariki. Aliporejea nyumbani Goldberg alipewa kazi na serikali ya Rais Thabo Mbeki ya kuwa mshauri katika wizara ya maji na uchumi wa misitu.

Mwanaharakati huyo leo anaifuatilia hali nchini mwake kwa wasi wasi mkubwa.Ni jambo la kusikitisha kwake kuona wazalendo wanaotumia bendera ya harakati za ukombozi kujitajirisha na kuyasaliti malengo aliyoyapigania na kuhatarisha maisha yake.Hata hivyo anaamini kwamba mapinduzi ya Afrika Kusini bado yamejificha katika awamu zake za mwanzoni.

Mwandishi:Stäcker, Claus

Tafsiri: Mtullya Abdu.

Mhariri: Josephat Charo