1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DHAKA:Serikali yasisitiza uchaguzi utafanyika bila dosari

26 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBVj

Serikali ya Bangladesh inayoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo inasisitiza kuwa ghasia na muda wa kutotembea uliotangazwa havitaathiri uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao.Kwa mujibu wa mshauri wa serikali Iftekhar Ahmed Chowdhury matukio hayo hayatafanya uchaguzi kutokuwa huru na haki.

Serikali inayosimamiwa na jeshi ilichukua jukumu la kuongoza nchi siku moja baada ya hali ya tahadhari kutangazwa na uchaguzi kufutwa baada ya kipindi cha miezi kadhaa ya ghasia kwasababu ya madai ya wizi wa kura.Jeshi linawakamata wanasiasa wa zamani katika juhudi za kupambana na ufisadi.Wanasiasa zaidi ya 150 wamekamatwa akiwemo waziri mkuu mmoja wa zamani.

Kulingana na mkuu wa jeshi ,uchaguzi mwengine umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao.Kiongozi wa serikali hiyo ya muda Fakhruddin Ahmed anatangaza kuwa hatua ya kutangaza hali ya kutotembea ililazimika kuchukuliwa ili kuepuka ghasia baada ya waandamanaji kupambana na polisi katika mji mkuu wa Dhaka na kwengineko. Mtu mmoja alipoteza maisha yake na wengine 300 kujeruhiwa katika ghasia zilizosibu kabla hali ya kutotembea kutangazwa.

Serikali ilisitisha kwa muda amri hiyo hapo siku ya Ijumaa na Jumamosi vilevile kutanganza kuwa hali hiyo itaendelea hii leo kwa kipindi cha saa 18.