1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DHAKA:Wahadhiri 4 wakamatwa

24 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWT

Majeshi ya usalama nchini Bangladesh yamewakamata wahadhiri wanne wanaodaiwa kuhusika na maandamano yaliyosababisha ghasia kati ya polisi na waandamanaji.Tukio hilo lilisababisha muda wa kutotembea kutangazwa katika miji sita.

Wahadhiri hao walikamatwa mapema hii leo kabla serikali kutangaza kuwa inasitisha kwa muda amri hiyo iliyowekwa baada ya siku tatu za ghasia nchini humo.Bangladesh ilikuwa chini ya sheria za dharura tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Harun ur Rashid mkuu wa Idara ya sayansi ya kijamii na Anwar Hossain mkuu wa idara ya sayansi ya biolojia ,katibu wa shirika la wahadhiri walikamatwa asubuhi ya leo.Wahadhiri hao wawili wanakashifu vitendo vya jeshi na serikali inayosimamiwa na jeshi tangu miezi saba iliyopita.Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mkwamo wa kisiasa uliopelekea uchaguzi mkuu kufutwa.

Wakati huohuo hali ya kawaida ilianza kurejea nchini humo huku barabara za mji zikijaa wateja wanaotafuta bidhaa za matumizi kabla muda wa kutotembea kutangazwa tena hii leo.

Maandamano hayo ya ghasia yalisababishwa na wanafunzi wa chuo kikuu cha Dhaka kudai kuondoka kwa majeshi waliolipiza kisasi kwa kuwarushia gesi ya machozi.Wakazi wengine wa mji walijiunga na waandamanaji hao hata baada ya serikali kuamua kukifunga chuo hicho cha Dhaka.

Ghasia hizo ni changamoto kubwa kwa serikali ya Fakhurdin Ahmed aliyetangaza muda wa kutotembea katika miji sita ukiwemo Dhaka tangu jumatano usiku ili kuepuka ghasia zaidi.