1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diane Rwigara: Mgombea urais Rwanda

4 Mei 2017

Rwigara alianza kufahamika mwaka 2015 baada ya baba yake kufa katika ajali ya gari inayoelezwa kuwa katika mazingira ya kutatanisha. Anataka kupambana na Rais Paul Kagame aliyeko madarakani tangu 2000.

https://p.dw.com/p/2cOL8
Diane Rwigara, mgombea urais Rwanda
Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

DW: Nini kimekupa hamasa kugombea?

Diana Rwigara: Kwa wakati huu yapo mambo mengi ambayo hayaendi ipasavyo katika sekta nyingi, kuna umasikini na ukosefu mkubwa wa ajira hususan miongoni mwa vijana, haki za watu zinakiukwa na wanyarwanda wengi wanajihisi kukosa usalama wa kisheria. Mambo hayo yote yamenisukuma kutaka kuyatafutia suluhisho, kwa sababu watu walio katika nyadhifa za juu, wanaopaswa kuwa wanayashughulikia, hawafanyi hivyo.

DW: Nimezungumzia masuala kama ukiukwaji wa haki za watu, na jana ulitaja mauaji kinyume cha sheria na watu kutoweka, wewe ikiwa utachaguliwa, vipi utaweza kuyaondoa matatizo hayo?

Diana Rwigara: Tunahitaji kwanza kuweza kuzungumzia matatizo yaliopo nchini mwetu. Nitakachokifanya ni kuwapa watu uhuru wa kujieleza, kwa sababu ni vigumu kuyatatua matatizo ambayo huwezi hata kuyazungumzia. Katika nchi nyingine angalau watu wana uhuru wa kuyazungumzia yasio sawa, lakini katika nchi yetu, kitu chenye kipaumbele hata kabla ya kuyatatua matatizo, ni kuwaacha kwanza waweze kuyasema na kuyajadili.

DW: Unaweza kuzungumzia vipi mazingira ya kisiasa nchini Rwanda kuelekea uchaguzi mkuu ujao, unayo matumaini kuwa wagombea wote watapata fursa sawa?

Diane Rwigara: Ninayo matumaini kwamba serikali yetu itatambua kuwa mambo hayawezi kuendelea kama yalivyo, kwamba huwezi kuwakandamiza watu kwa muda mrefu. Ni matumaini yangu kuwa katika uchaguzi huu wagombea wote watapewa nafasi ya kufanya kampeni na kunadi sera zao, na pia kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na wenye uwazi.

DW: Wewe bado una umri mdogo tu wa miaka 35, hudhani kuwa kukosa uzoefu kutakuwa changamoto kwako katika kukabiliana na mwanasiasa mzoefu kama Paul Kagame?

Diana Rwigara: Mimi naamini kuwa unavyokaa madarakani muda mrefu, ndivyo unavyokwenda mbali ya wananchi wa kawaida. Watu hutaka kuifanya siasa kuwa kitukigumu, lakini siasa ni kuelewa masuala ya nchi. Mimi nimepitia katika matatizo makubwa maishani mwangu, nimewaona watu wakipita katika matatizo chini ya utawala huu. Sasa nani anaweza kuyatatua vyema zaidi matatizo ya watu kuliko mtu ambaye ameshuhudia kinachoendelea?

Diane Shima Rwigara, mwenye nia ya kugombea urais nchini Rwanda, alikuwa akizungumza na Bruce Amani

Mwandishi: Daniel Gakuba/Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga