1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dikteta wa zamani wa Chad Hissen Habre kupandishwa kizimbani

19 Julai 2015

Robo karne baada ya dikteta katili kabisa nchini Chad Hissene Habre kuangushwa kutoka madarakani, wengi katika taifa hilo wanaridhika kumuona hatimaye akifikishwa mahakamani kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

https://p.dw.com/p/1G18k
Hissene Habre vor Gericht
Dikteta Hissen HabrePicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Hata leo hii, baadhi ya watu wanashusha sauti zao wanapopita mbele ya jengo la makao makuu ya zamani ya polisi wa siri wa Habre, kikosi cha mamlaka ya usajili na usalama DDS, katika mji mkuu N'Djamena, ambako utesaji ulikuwa ni jambo la kawaida wakati wa utawala wa dikteta huyo katika miaka ya 80.

"Jela hiyo ilikuwa ni jahanamu," amesema Abdourahmane Gueye , mmoja kati ya wahanga 4,000 ambao ni sehemu ya kesi dhidi ya Habre, ambaye kesi yake inaanza rasmi katika mji mkuu wa Senegal , Dakar kesho Jumatatu (20.07.2015).

Senegal Prozess gegen Hissene Habre in Dakar Pressekonferenz
Wahanga wa utesaji katika utawala wa zamani wa dikteta Hissen Habre mjini DakarPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Blackwell

Gueye , Msenegali pekee ambaye amefungua kesi hiyo dhidi ya Habre, ameshutumiwa kwa ujasusi mwaka 1987 na kufungwa kwa miezi saba. Akiwa jela, yeye pamoja na wafungwa wengine 40 walijazwa katika chumba ambacho hakina taa.

"Watu wamefariki katika chumba hicho," amesema. Habre , mwenye umri wa miaka 72, anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na utesaji wakati wa utawala wake wa miaka minane akiwa madarakani kati ya mwaka 1982 na 1990. Makundi ya haki za binadamu yanasema watu 40,000 wameuwawa wakati wa utawala wake, ambao ulikandamiza kwa nguvu wapinzani wa kisiasa na watu kutoka makundi mengine ya kikabila ambayo ni tofauti ya kabila la Habre la Gorane. Souleymane Guangueng , ambaye ni mhasibu , amesema ameona "vifo vitatu ama vinne" kila siku mikononi mwa polisi hao wa siri, ambao walimtia mbaroni mwa muda wa miaka miwili na nusu kuanzia Agosti mwaka 1988.

"Mateso yalikuwa ya kila aina, kiroho na matumizi ya nguvu," amesema Guengueng. Souleymane Guangueng alikuwa tu ametoka hospitali baada ya operesheni wakati alipokamatwa. Akiwa kizuwizini, "waliniacha nife, nilikuwa katika chumba bila matibabu, hata bila chakula."

Hissene Habre
Dikteta Hissen HabrePicha: picture-alliance/dpa

Hivi sasa, anasema , anataka kumtazama Habre usoni katika chumba cha mahakama. "Hata kama hatasungumza, analazimika kusikiliza kile tutakachosema na atuone kwa macho yake." Habre anakataa kutambua uhalali wa mahakama hiyo na mawakili wake wanasema hatafika mahakamani, hata kushiriki pia. Lakini baadhi ya wale walioteseka chini ya utawala wake wanataka aelezee binafsi mahakamani madhila ambayo yamesababisha makovu ya kudumu na vilema.

"Anapaswa kuwa jasiri vya kutosha kutuambia kila kitu kilichotokea," amesisitiza Issaka Ramat, mwanaharakati wa kisiasa.

Idriss Deby Präsident Tschad
Rais wa sasa wa Chad Idriss DebyPicha: AFP/Getty Images/Seyllou

"Leo , historia inamhukumu. Tutaona kile atakachosema mahakamani."

Chad katika miezi ya hivi karibuni imekuwa lengo la mashambulizi ya mabomu pamoja na uvamizi wa kundi la Boko Haram, kutoka Nigeria. Lakini miaka ya giza kabla ya rais wa sasa Idriss Deby kumwangusha kutoka madarakani Habre haijasahaulika katika mji mkuu. Vilio vya kupatikana haki vimesikika mara kwa mara katika majadiliano mjini N'Djamena. "Kesi hii inasubiriwa kwa hamu na watu wa Chad," mfanyabiashara Youssouf ameliambia shirika la habari la AFP.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar