1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dimba la AFCON kuzishirikisha timu 24

Bruce Amani
19 Julai 2017

Dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON limetanuliwa hadi timu 24 na kusogezwa katika tarehe za Juni na Julai lakini litaendelea kuandaliwa kila baada ya miaka miwili. Kwa sasa linazishirikisha timu 16

https://p.dw.com/p/2goe6
Fußball | Africa Cup 2017 | Gabun vs Guniea Bissau
Picha: Getty Images/AFP/G. Bouys

Hayo ni kutokana na mapendekezo yaliyofanywa kuhusu dimba hilo katika mkutano wa wadau ulioandaliwa mjini Rabat nchini Morocco. Uamuzi huo lazima lakini uidhinishwe na kamati kuu ya Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF, katika mkutano wake wa siku mbili mjini Rabat.

Mapendekezo hayo yanayosubiriwa kuidhinishwa rasmi, yalifanywa katika warsha kuhusu mustakabali wa wa kinyang'anyiro hicho ambayo ilijumuisha viongozi wakuu wa CAF.

Dimba la AFCON limekuwa likizusha utata kwa sababu ya kuandaliwa Januari, katikati ya msimu wa ligi kuu za kandanda Ulaya. Wachezaji wengi wa AFCON hutoka katika vilabu vya Ulaya na mara nyingi hujikuta katika hali ya vuta nikuvute kati ya klabu na nchi.

Ongezeko la timu linafuatia utanuzi wa dimba la ubingwa wa Ulaya – Euro mwaka jana, ambao wachambuzi wa Afrika walisema ulikuwa wa kufana.

Rais wa Shirikisho la Kandanda la Nigeria Amaju Pinnock, ambaye pia ni mwanachama wa kamati kuu ya CAF anasema "kutoka kwa mtazamo wa michezo, itatoa fursa zaidi kwa wachezaji kutoka kote Afrika. Itaongeza mapato kwa CAF na tunaweza kuongeza mara tatu zaidi mapato yetu. Pia italazimisha maendeleo zaidi ya miundi mbinu”.

Mwandishi: Bruce  Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo