1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dimba la olimpik laanza leo

5 Agosti 2008

Dimba la wanawake la olimpik laanza leo kwa mabingwa wa dunia Ujerumani wakicheza na Brazil.

https://p.dw.com/p/Eqyr

Masaa 48 kabla michezo ya 29 ya olimpik kufunguliwa rasmi ijumaa hii, mashindano ya kabumbu ya olimpik, yanaanza leo (jumatano) kwa mabingwa wa dunia-timu ya wanawake ya Ujerumani ikipambana na ile ya Brazil,ikiongozwa na stadi wao "Marta"- mchezaji bora wa mwaka wa dimba wa Brazil.

Alhamisi, dimba la wanaume litaanza huku timu 3 za Afrika- Nigeria , Kamerun na Ivory Coast zikiania pia taji la olimpik la dimba.Nigeria ilikwisha tawazwa mabingwa wa olimpik huko Atlanta,1996 wakati simba wa nyika-kamerun walitwaa ubingwa katika michezo ya Sydney,Australia, 2000.

►◄

Mabingwa wa olimpik upande wa wanawake ni Marekani na wana miadi pia leo na Norway.Marekani iliilaza Brazil katika finali ya Olimpik ya Athens, Ugiriki miaka 4 iliopita.

Lakini , ni changamoto kati ya mabingwa wa dunia na makamo-bingwa -Ujerumani na Brazil inayokodolewa zaidi macho hii leo.Kwani, Brazil ina nafasi leo ya kulipiza kisasi chake kwa kunyimwa kombe la wasichana wa Ujerumani huko huko China, mwaka uliopita baada ya stadi wa Brazil Marta kukosa mkwaju wa penalty.

Marta,mwana soka wa mwaka wa Brazil, ameahidi mara hii kurekebisha mambo na kurejea Rio de Jeneiro na medali ya kwanza ya dhahabu kutoka dimba la olimpik.

wasichana wa Ujerumani baada ya kutawazwa mabingwa wa dunia,wamepania nao kutawazwa mabingwa wa olimpik.Na wanajua njia ya finali ya olimpik inapitia Brazil.Kwahivyo, lazima watambe leo.Ujerumani iliikomea Brazil mabao 2:0 katika finali ya kombe la dunia ,2007 .Lakini, mla ni mla leo, mla jana-kala nini ?

Mabingwa wa olimpik Marekani wana miadi na Norway katika kundi G na Japan inaumana na New Zealand katika kundi hili. Wenyeji China wanapambana na sweden huko Tianjin.

Baada ya timu za akina dada kuondoka uwanjani,kesho itakua zamu ya timu za wanaume : Afrika inawakilishwa na timu 3-mabingwa wake 2 wa olimpik -Nigeria na simba wa nyika kamerun na timu ya 3 ni tembo wa ivory Coast au Corte d'Iviore.

Ivory Coast iko kundi A ikicheza kesho mjini Shanghai na Argentina wakati Australia ikiumana na serbia katika kundi hili.

Kundi B -mabingwa wa olimpik wa 1996 huko Atlanta,Georgia-Nigeria wana miadi na Holland.Mabingwa wa olimpik Marekani watatoana jasho na Japan huko Tianjin.

Kundi C litakalocheza huko Shenyang ni kati ya Brazil na Ubelgiji na wenyeji China watapapurana na New Zealand.

Kundi D litacheza mechi zake huko Qinhuangdao ambako Itali wataumana na Hondurus na simba wa nyika Kamerun, wana miadi na korea.

Swali ni timu gani 2 zitakutana finali ?

Je, ni timu ya kiafrika na ya Amerika kusini au itakua kati ya madume 2 wa Amerika kusini:Brazil na Argentina ?

kumekuwa na kitandawili kimoja ambacho hakijafumbuliwa hadi tulipoingia mitamboni ikitumainiwa kauli ya mwisho kutolewa leo jumatano:

Klabu za dimba za Ulaya kama vile FC Barcelona ya Spian, Werder Bremen na Schalke zikipigana hata jana kuwabakisha nyumbani mastadi wao kama vile muargentina Lionel Messi-wabrazil Diego na Rafinha wasishiriki katika olimpik na wazichezee Ligi zao ukianza msimu mpya mwishoni mwa wiki ijayo.

Hata ikiwa Lionel Messi itaamuliwa leo hawezi kushiriki, Argentina kama Brazil ina chipukizi wengi wapya wa dimba kuweza kuwachezesha.

kuwachezesha.Argentina pia ina wajuzi kama Juan Roman Riquelme,stadi wa Real Madrid Sergio Aguero na javier Maschereno wa Fc Liverpool ya Uingereza.

Brazil imehakikishiwa kuweza kucheza mastadi wake kama Anderson wa Manchester united,Alexandre Pato wa AC Milan, mlinzi wa Real Madrid Marcelo pamoja na wachezaji 3 waliopindukia umri wa miaka 23 kama vile Ronaldinho aliejiounga msimu mpya na Ac milan. Mastadi wengine wa timu kama Holland na marekani ni pamoja na Roy makaay kutoka Feynoord Rotterdam na freddy Adu anaeichezea Benfica.

Macho yatakodolewa timu 2 za Ulaya-Itali na Holland kujua iwapo zaweza kuizuia Brazil au argentina kutoroka na taji la olimpik.

Brazil haikuwahi kutawazwa mabingwa wa olimpik na wanadai huu mwaka wao.Katika timu 3 za Afrika, ni Ivory Coast pekee haikuwahi kuvaa taji la Olimpik ,lakini ili iweke matumaini itabidi kwanza kesho kutamba mbele ya Argentina.