1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dirisha la uhamisho wa wachezaji lafungwa

31 Januari 2014

Kipindi cha usajili wa wachezaji wapya, kimefikia tamati na kuna wale waliofaidika na wale walioachwa wakijikuna vichwa. Katika ligi Ujerumani, timu iliyohitaji sana wachezaji wapya ni Borussia Dortmund

https://p.dw.com/p/1B0KO
Milos Jojic
Picha: Getty Images

Dortmund kwa sasa inakabiliwa na matatizo chungu nzima kutokana na idadi ya wachezaji wake waliopata majeraha. Imebidi vijana hao wa njano wamsajili kiungo Mserbia Milos Jojic. Usajili wa Jojic aliyehamia Dortmund kutoka Partizan Belgrade na usajili wa Mpoland Ludovic Obraniak katika klabu ya Werder Bremen kutoka Girondins Bordeaux ndio shughuli pekee iliyofanywa katika dakika za mwisho mwisho wakati kipindi cha usajili wa wachezaji cha Januari kilipofikia kikomo jana. Kwa jumla, katika kipindi hiki, timu 18 za Bundesliga ziliwasajili wachezaji 32 na kuwauza 37. usajili mkubwa ni wa Mbelgiji Kevin De Bruyne aliyejiunga na VfL Wolfsburg kutoka Chelsea kwa kiasi cha euro milioni 20. Mkorea Kusini Koo Ja-Cheol alihama Wolfsburg na kujiunga na Mainz kwa kiasi cha euro milioni tano.

Schalke ilimtuma kiungo Mmarekani Jermaine Jones katika klabu ya Besiktas ya Uturuki kwa mkopo wakati nao miamba Bayern wakitosheka na kikosi chao…ijapokuwa walimwacha beki wao Jan Kirchoff akajiunga na Schalke kwa mkopo.

Kiungo Jermaine Jones amejiunga na Besiktas kwa mkopo kutoka Schalke
Kiungo Jermaine Jones amejiunga na Besiktas kwa mkopo kutoka SchalkePicha: Christof Koepsel/Bongarts/Getty Images

Tukiwachana na mambo ya uhamisho wa wachezaji, sasa tuangalia ligi iko vipi? Na suali kuu linaloulizwa na kila shabiki ni, nani anayeweza kuipunguza kasi ya Bayern Munich?

Huenda wanaongoza msimamo wa ligi na pengo la pointi 13 dhidi ya nambari mbili, na wamecheza mechi 43 mfululizo bila kushindwa, lakini kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola ameionya timu yake kusalia makini. Miamba hao wa Bavaria wanawaalika Eintracht Frankfurt kesho Jumapili katika uwanja wa nyumbani Allianz Arena huku wachezaji Arjen Robben na Frank Ribery wakirejea kikosini baada ya kupona majeraha ya miguu.

Guardiola ametoa onyo hilo kuafuatia mchuano wa wiki wiki iliyopita ambao walitokwa jasho kwa kushinda magoli mawili kwa moja dhidi ya Stuttgart. Bayer Leverkusen na Borussia Dortmund zimekiri kuwa zinapigania nafasi ya pili tu kwa sababu tayari taji la ligi limewaponyoka. Leverkusen wanawaalika Stuttgart hii leo. Nambari nne Borussia Moenchengladbach ambao wana pointi sawa na Dortmund wanacheza leo dhidi ya Hanover.

Katika mechi nyingine za leo, Schalke 04 v VfL Wolfsburg, Hoffenheim v Hamburg, Mainz v Freiburg, Augsburg v Werder Bremen. Kesho Jumapili, Hertha Berlin watafunga kazi dhidi ya Nuremberg.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu