1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola bilioni 1 kukatwa gharama za misaada ya kiutu

Mohammed Khelef24 Mei 2016

Wakuu wa serikali za mataifa yanayoshiriki mkutano wa kilele juu ya Misaada ya Kibinaadamu mjini Istanbul wamekubaliana na mashirika ya misaada ya kiutu kukata gharama za uendeshaji wa masuala ya misaada.

https://p.dw.com/p/1ItRM
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, akizungumza kwenye Mkutano wa Kilele wa Msaada wa Kibinaadamu unaofanyika Instanbul, Uturuki.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, akizungumza kwenye Mkutano wa Kilele wa Msaada wa Kibinaadamu unaofanyika Instanbul, Uturuki.Picha: Reuters/O. Orsal

Mkutano huo ulioanza jana na unaoyakutanisha mataifa 21 yanayofadhili shughuli za kibinaadamu na mashirika 16 ya misaada umepitisha azimio la kupunguza kiwango cha ukosefu wa ufanisi na kulainisha vikwazo wanavyokumbana watoaji na wapokeaji wa misaada ya kibinaadamu kote duniani.

Endapo azimio hilo litatekelezwa kikamilifu, itasaidia kujaza pengo la dola bilioni 15 kwa mwaka katika kukabiliana na mahitaji ya dharura kwa zaidi ya watu milioni 125 duniani kote, sambamba na kuunda mfumo utakaowezesha kupatikana kwa fedha zaidi kutoka kwa wafadhili wengine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema makubaliano hayo, ambayo yanajumuisha vipengele 51, yatawezesha msaada kuwafikia walengwa haraka zaidi na kwa wakati zaidi, wakiwemo waathirika wa majanga ya kimaumbile yaliyodumaza maendeleo ya kisiasa kwengineko duniani.

"Kitisho cha majanga kiliyazidi nguvu mafanikio ya kisiasa mwaka jana, kama ule Utaratibu wa Sendai ambao ulitaka kupunguzwa kwa majanga, Ajenda ya 2030 juu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu na Makubaliano ya Paris juu ya Mabadiliko ya Tabia Nchi. Kwa hivyo lazima tuyaheshimu makubaliano haya na kutimiza ahadi zetu. Na huo ndio msingi muhimu wa kikao hiki."

Makubaliano ya kihistoria

Makamu wa rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya anayehusika na bajeti na rasilimali watu, Kristina Georgieva, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba vikwazo vinavyoyakumba mashirika ya misaada duniani vinakula zaidi ya asilimia 15 ya fedha yanayopokea kutoka kwa wafadhili.

Wajumbe wa Mkutano wa Kilele wa Msaada wa Kibinaadamu unaofanyika Instanbul, Uturuki.
Wajumbe wa Mkutano wa Kilele wa Msaada wa Kibinaadamu unaofanyika Instanbul, Uturuki.Picha: picture-alliance/AA/M. Pala

Georgieva, ambaye ameshiriki kuandaa makubaliano haya, amesema anatazamia sasa rasilimali zaidi zitafikishwa kwa watu wenye mahitaji hasa, wakiwemo wafanyakazi wenyewe wa mashirika ya misaada ambao wanahatarisha maisha yao kwa kuwa mstari wa mbele wa mapambano.

Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Alexander De Croo, ameyaita makubaliano hayo kuwa ya kihistoria na ambayo yatageuza mfumo mzima wa misaada ya kiutu duniani.

"Watu wanateseka kwa kuwa kanuni za msingi za sheria za kimataifa juu ya ubinaadamu zinakiukwa kila mara. Mkutano huu wa kwanza kabisa wa kihistoria juu ya ubinaadamu unaweza kubadilisha hilo. Ubinaadamu wa kesho uko kwenye makubaliano tunayoyapitisha leo hapa."

Makubaliano hayo yanayoungwa mkono na mataifa makubwa yanayofadhili shughuli za misaada, zikiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Japan, yanayataka pia mataifa hayo kurahisisha upatikanaji fedha zao na kuwekeza kwenye miradi ya muda mrefu ambayo inayawezesha mashirika ya misaada kujihusisha na mengi zaidi kando ya kusambaza tu bidhaa na vifaa kwa waathirika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf