1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola la Kiislamu lamuua mwanaakiolojia wa Palmyra

Admin.WagnerD19 Agosti 2015

Kundi la Dola la Kiislamu limemuua mwanaakiolojia wa Palmyra aliyekataa kuondoka katika mji huo mkongwe tangu lilipouteka Mei mwaka huu. Watu 16 wameuawa leo (19.08.2015) katika shambulizi dhidi ya vikosi vya Wakurdi.

https://p.dw.com/p/1GHub
Khaled al-Asaad
Mwanaakiolojia wa Palmyra, Khaled al-Asaad aliyechinjwa na Dola la KiislamuPicha: picture alliance/AP Photo

Mkuu wa mambo ya kale nchini Syria Maamoun Abdulkarim ameliambia shirika la habari la afp kwamba alikuwa amemhimiza Khaled al-Asaad aondoke Palmyra, lakini akakataa kata kata. Abdulkarim amesema mwanaakiolojia huyo ameuawa kwa kuchinjwa jana mchana mjini Palmyra, katikati mwa jimbo la Homs.

Picha zilizoonekana kuonyesha mwili wa Asaad ukiwa umefungwa kwenye mlingoti mjini humo zilisambazwa katika mtandao wa intaneti na wafuasi wa kundi la Dola la Kiislamu IS. Alikuwa mkuu wa mambo ya kale mjini Palmyra kwa miaka 50 na alikuwa amestaafu kwa miaka 13. Abdulraham amesema mwili wake umetundikwa katika magofu ya zamani ya mji huo baada ya kukatwa kichwa, lakini picha ya mtandaoni ilionyesha maiti yake ikiwa imefungwa kwenye mlingoti wa taa.

Alama ilitundikwa katika maiti hiyo iliyoitambulisha kuwa ya Asaad na kumshutumu kwa kuwa mfuasi wa serikali kwa kuiwakilisha Syria katika mikutano nje ya nchi na makafiri, pamoja na kuwa mkurugenzi wa 'sanamu' za Palmyra. Asaad alikuwa na umri wa miaka 81.

Shambulizi laua wapiganaji wa Kikurdi

Wakati haya yakiarifiwa, Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binaadamu la Syria limesema mlipuko katika mji wa Qamishli limewaua wanachama 10 wa vikosi vya Wakurdi vinavyoitwa Asayish, na raia sita.

Syrien Kurdische Kämpfer in Tel Abyad
Wapiganaji wa Kikurdi wa Syria wakiwa Tel AbyadPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Mkuu wa shirika hilo lenye makao yake jijini London Uingereza, Rami Abdel Rahman, amesema mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliyekuwa ndani ya gari ameyashambulia makao makuu ya vikosi vya Wakurdi katika eneo hilo.

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulizi hilo katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao wa intaneti, likisema mshambuliaji huyo alitumia tangi la maji lililokuwa limejazwa vilipuzi kuweza kuingia katika kambi ya wapiganaji Wakurdi.

Wapiganji wa Kikurdi wa Syria wamekuwa miongoni mwa makundi yaliyofanikiwa sana katika mapambano dhidi ya Dola la Kiislamu katika maeneo ya kaskazini ya taifa hilo. Kundi hilo la wapiganaji wa jihadi limezishambulia ngome za wapiganaji wa Qamishli na makundi mengine ya kikurdi katika operesheni za mashambulizi ya kujitoa muhanga katika siku zilizopita.

Abdel Rahman amelieleza shambulizi la leo kuwa kubwa na kusema takriban raia kumi na wanne wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape

Mhariri:Daniel Gakuba