1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola la Kiislamu ni nani?

Abud Mtullya1 Desemba 2015

Tangu mwaka wa 2013 wametokea magaidi wanaoendesha harakati kwa lengo la kuunda nchi ya kiislamu. Ukweli ni kwamba nchi za Magharibi zimechangia kuibuka kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu ama IS.

https://p.dw.com/p/1HFFA
Wapiganaji wa Dola la Kiislamu
Picha: picture-alliance/abaca

Muda mfupi tu baada ya dunia kupata habari juu ya kufanyika mashambulio ya kigaidi mjini Paris, mashabiki wa kundi la magaidi wanaoitwa Dola la Kiislamu waliyashangilia mauaji hayo katika mitandao ya kijamii. Na katika mchana wa jumamosi, yaani siku moja baada ya mauaji hayo, Dola la Kiislamu lilitoa taarifa kudai kuwa watu wao ndio walihusika na shambulio hilo.

Na hata kama ilikuwa bado haijathibitishwa, hakuna mwenye mashaka kuwa madai yao yalikuwa ya kweli.

Baadhi ya wataalamu sasa hawazungumzii tena juu ya kikundi fulani tu cha watu, bali wanazungumzia juu ya kuwepo vuguvugu la kijamii na kisiasa kuhusiana na Dola la Kiislamu. Mtaalamu wa masuala ya Uislamu Christoph Günther kutoka chuo kikuu cha Leipizig ameeleza hayo.

Kundi laundwa Iraq

Mnamo mwaka wa 2013 wakati ambapo vita vya nchini Syria vilishaingia katika mwaka wa pili, na wakati ambapo nchi za magharibi zilikuwa bado haziamua kuchukua hatua za kijeshi, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yalikuwa yanatoa taarifa juu ya unyama na mauaji ya halaiki yaliyokuwa yanafanywa na magaidi wa Dola la Kiislamu. Watu walikuwa wanauliwa wakati walipokuwa usingizini na wakati mwingine walikuwa wanauliwa kwa kupigwa risasi kwa sababu za kupuuzi tu.

Tangu mwaka mmoja na nusu magaidi wa Dola la Kiislamu wamekuwa wanaiweka dunia roho juu! Na hasa tangu walipoanza kuonyesha katika kanda za video jinsi walivyokuwa wanawachinja waandishi wa habari wa nchi za magharibi, wafanyakazi wa mashirika ya misaada na waasi wanaopamba na utawala wa Assad.

Kiongozi wa Dola la Kiislamu, Abu Bakr al-Baghdadi
Kiongozi wa Dola la Kiislamu, Abu Bakr al-BaghdadiPicha: picture-alliance/AP Photo

Wauaji hao walikuwa wanaonekana na visu mikononi na wengine walikuwa wanazungumza lafudhi asilia ya kiingereza na wengine walikuwa na lafidhi ya kifaransa. Kwa kuwachinja binadamu wenzao mbele ya kamera, magaidi wa Dola la Kiislamu wanatumia vyombo vya habari kwa njia ya ukatili. Magaidi hao wamekuwapo kwa zaidi ya miaka 10 wakiendesha harakati zao katika nchi kadhaa.

Magaidi wa IS wanatokana na kijitawi cha kundi jingine la kigaidi la al-Qaeda kutoka Iraq. Mnamo mwaka wa 2003 majeshi ya Marekani kwa kushirikiana na ya nchi ningine aliivamia Irak na kumtimua Saddam Hussein. Watu wake waliokuwa wanamuunga mkono, yaani Wasuni pia waliondolewa serikalini, kuanzia majasusi hadi walinzi maalumu. Wengi walikamatwa na kufungwa jela. Maalfu kwa maalfu ya Wasuni wa Iraq, ikiwa pamoja na majenerali, maafisa, askari wa kawaida na watumishi serikali waliwekwa kandoni kabisa.

Günther Meyer kutoka kituo cha utafiti wa masuala ya nchi za kiarabu kwenye chuo kikuu cha Mainz, amesema thama na uvamizi uliofanywa na Marekani wasingelitokea magaidi wa Dola la Kiislamu.

Vita vya Syria vyawafaidisha

Wafuasi wa Saddam Hussein wa hapo awali walijiunga ili kuanzisha upinzani dhidi ya Marekani. Kundi la al-Qaeda lilianzishwa nchini Iraq, chini ya uongozi wa Abu Musab al-Zarkawi. Na kuanzia wakati huo Iraq imekuwa inawavutia wanajihadi. Baada ya al-Zarkawi kuuliwa mnamo mwaka wa 2006 magaidi hao walibadilisha jina na kuanza kujiita "Dola la Kiislamu nchini Irak (ISI).“

Mwanzoni mwa mwaka wa 2013, kundi hilo lilianza kujiingiza nchini Syria na kujitandaza na ndipo lilipobadilisha jina na kujiita Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq, ISIS. Lakini palitokea mfarakano na baina ya kundi la al-Qaeda na al-Nusra. Hadi wakati huo magaidi wa al-Qaeda walikuwa wamepata mafanikio makubwa nchini Syria.

Kundi la al-Nusra lilikataa kumtii al-Baghdadi aliechukua uongozi. Mengi hayajulikani juu ya mtu huyo ambae jina lake la kweli ni Ibrahim al-Badri. Kinachojilikana ni kwamba alizaliwa mjini Baghdad na kwamba anatokea katika nasaba ya kimasikini.

Sasa al-Baghdad anaongoza harakati za kupigania kuundwa nchi ya kiislamu, ikiwezekana katika Syria, Iraq, Lebanon na Palestina. Mwishoni mwa mwaka wa 2013 wapigananji wa Dola la Kiislamu walijitandaza hadi katika mji wa Raqqa na kujenga ngome. Na walianzisha kujitandaza, kutoka katika jimbo hilo.

Mosul yatekwa

Mtaalamu wa masuala ya nchi za kiarabu, Günter Meyer, amesema kujitandaza kwa magaidi wa Dola la Kiislamu kulianza hasa baada ya mji wa Mosul wa kaskazini mwa Irak kutekwa. Mji huo ulikuwa ngome ya wafuasi wa zamani wa Saddam Hussein. Baada ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu kuuteka na kuudhibiti mji huo, majenerali wa zamani wa Iraq ambao ni Wasuni walijiunga na wapiganaji hao.

Kutokana na siasa za kibaguzi za aliekuwa Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ambae ni Mshia wapiganaji hao wa Dola la Kiislamu walitaka kulipiza kisasi. Pamoja na hatua nyingine walipora mamilioni kwenye Benki Kuu ya mjini Mosul.

Mwaka jana walisonga mbele kuelekea mji wa Baghdad. Wanajeshi wa Irak waliokuwa dhaifu waligwaya mbele ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu. Wanajeshi hao walitimua mbio bila ya kujitetea na kuzitelekeza silaha za kisasa zilizotekwa na magaidi wa ISIS.

Kiongozi wa Dola la Kiislamu, al-Baghdadi, alitangaza utawala wa kihalifa katika maeneo yaliyotekwa na magaidi wake. Alilibadilisha jina la wapiganaji wake na kuwa Dola la Kiislamu. Aliondoa mipaka yote na kuanzisha utaratibu wa sheria za kiislamu. Watu wengine, wakristo na wayahudi waliuliwa au waligeuzwa watumwa. Vijana wa kiislamu na wale waliosilimu kutoka barani Ulaya kote walienda Irak na Syria ili kujiunga na Dola la Kiislamu na kupigana pamoja nao bega kwa bega.

Vijana wenye itikadi kali wajikusanya

Kwa mujibu wa wataalamu, vijana kadhaa kutoka Ujerumani pia wamekwenda kujiunga na Dola la Kiislamu nchini Syria na Irak. Lakini wanachokifanya hasa hakijulikani vizuri, iwapo wanashiriki katika mapigano au la. Kwa mujibu wa taarifa watu 50,000 wanapigana kwa niaba ya Dola la Kiislamu.

Wanaamini kwamba wanao wajibu wa kupigana na ndugu zao ili kuwalinda dhidi ya Washia. Mtaalamu wa masuala ya nchi za kiarabu Günter Meyer amesema vijana hao pia wanavutiwa na fedha wanazolipwa. Katika harakati zao za miezi ya hivi karibuni wapiganaji wa Dola la Kiislamu waliviteka visima vya mafuta na gesi chungu nzima

Watu hao waliuza zana za kijeshi walizoziteka, walitoza kodi katika maeneo waliyoyateka na waliwalazimisha watu walipe fedha. Kutokana na njia hizo wameweza hadi sasa kujigharimia wenyewe badala ya kuwategemea wafadhili kutoka nchi za kiarabu.

Nani aweza kuipiga IS?

Kutokana na fedha walizonazo Dola la Kiislamu hawana matatizo ya kupata silaha kwa kupitia Uturuki na Lebanon. Na wataalamu wanasema Dola la Kiislamu lina nguvu kubwa za kijeshi. Lakini magaidi wa Dola la Kiislamu wamezuiwa kuteka maeneo zaidi. Pana sababu kadhaa zilizochangia

Wanajeshi wa Peshmerga wapambana na Dola la Kiislamu Iraq
Wanajeshi wa Peshmerga wapambana na Dola la Kiislamu IraqPicha: picture-alliance/dpa/T. Rassloff

Kwanza ni uamuzi wa nchi za magharibi kuwapa silaha wapiganaji wa kikurdi wa Peshmerga kaskazini mwa Irak. Ujerumani pia imewapa Peshmerga silaha. Harakati za wapiganaji wa kikurdi kaskazini mashariki mwa Syria pia zimetoa mchango katika kuwazuia magaidi wa Dola la Kiislamu.

Na nchi zilizofungamana chini ya uongozi wa Marekani pia zimekuwa zinazishambulia ngome za Daish kwa ufanisi kwa miezi kadhaa sasa. Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya Uislamu Christoph Günther kutoka chuo kikuu cha Leipzig hana uhakika iwapo itawezekana kuwashinda kijeshi wapiganaji wa Dola la Kiislamu katika kipindi cha muda mrefu.

Itawezekana kuwarudisha nyuma kwa mashambulio ya ndege na mengine, lakini njia hiyo haitafua dafu mbele ya itikadi ya watu hao. Mtaalamu huyo na wengine wengi wanaamini kwamba ni Wasuni wenye siasa za wastani wa sehemu hizo watakaoweza kuwashinda Dola la Kiislamu daima. Idadi kubwa ya watu katika sehemu hiyo wanawapinga magaidi wa Dola la Kiislamu na pia hawakubaliani na itikali kali yao.

Mkuu wa kitengo cha mitaala ya Mashariki ya kati na Afrika kwenye chuo kikuu cha Humboldt-Viadrana mjini Berlin, Udo Steinbach, amesema ikiwa watu hao wenye siasa za wastani wataunga itawzekana kuwashinda magaidi wa Dola la Kiislamu kijeshi.

Waandishi: Shtrauchler, Nastassja/Hodali, Diana

Mfasiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Elizabeth Shoo