1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dominique Strauss-Kahn kubakia rumande

17 Mei 2011

Mahakama ya Manhattan jijini New York imemkatalia dhamana Meneja Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa, Domonique Strauss-Kahn, ambaye ameshitakiwa kwa makosa ya kujaribu kumbaka mhudumu wa hoteli.

https://p.dw.com/p/11HhS
Dominique Strauss-Kahn, kulia, na wakili wake, Benjamin BrafmanPicha: dapd

Kwa kukataliwa kwa dhamana yake, sasa Strauss-Kahn alipaswa kupelekwa kwenye jela maarufu jijini New York ya kwenye kisiwa cha Rikers. Akiwa mahakamani hapo, mzee huyu wa miaka 62 alionekana mchofu na mwenye fadhaa, huku akiwasikiliza waendesha mashitaka wakiorodhesha mkururo wa makosa anayoshitakiwa nayo kwa tuhuma za shambulio la aibu katika hoteli moja ya kifahari jijini New York.

Mawakili wake walijaribu kupigania mteja wao aachiwe kwa dhamana ya fedha taslimu dola za Kimarekani milioni moja, lakini upande wa mashitaka ulifanikiwa kumshawishi jaji kwamba kama akipewa dhamana, Strauss-Kahn atakimbilia Ufaransa, na jaji huyo akaamuru arudishwe kizuizini.

Wakati wote majibizano yakiendelea baina ya mawakili wa pande zote mbili, Strauss-Kahn hakusema kitu zaidi ya kukana makosa yote sita, na baada ya jaji kutangaza uamuzi wake, maafisa wa polisi walimchukua na kumpeleka kwa muda kwenye jela ya The Tombs, ambapo maafisa wamesema kwamba baadaye angelihamishiwa kwenye jela maarufu kwenye kisiwa cha Rikers.

Uamuzi huu wa kumkatalia Strauss-Kahn dhamana, umewafadhaisha sana mawakili wake, ambapo mmoja wao, Ben Brafman, aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, kwamba mapambano ya kutafuta haki ya mteja wao ndio kwanza yameanza na kwamba wataukatia rufaa uamuzi huo:

"Tutathibitisha kwamba Bwana Strauss-Kahn hana makosa. Lengo lake kubwa ni kusafisha jina lake na kujijengea upya heshima yake."

Endapo atapatikana na hatia, mkuu huyu wa taasisi kubwa kabisa ya fedha duniani, anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 jela. Mlalamikaji wake, mwanamke wa miaka 32, anasema kwamba Strauss-Kahn alimshambulia wakati alipoingia kusafisha chumba chake cha kifahari katika hoteli ya Sofitel karibu na Times Square, jijini New York.

Waendesha mashitaka waliiambia mahakama kwamba Strauss-Kahn aliyekuwa maliwatoni wakati mhudumu huyo akiiingia chumbani kwake, alitoka na kuukomea mlango kwa ndani kumzuia asikimbie.

Kwa vyovyote vile, hata mahkama ikimsafisha na tuhuma hizi, tayari kesi yenyewe imemdhalilisha mwanasiasa huyu ambaye hadi Jumamosi iliyopita alikuwa akionekana kama mgombea imara katika uchaguzi wa urais wa Ufaransa wa hapo mwakani.

Strauss-Kahn amejizolea sifa kama kiongozi wa IMF, ambaye aliingia madarakani wakati uchumi wa dunia ulipokuwa unakumbwa na mtikisiko mkubwa hapo mwaka 2007.

Barani Ulaya, ambako mataifa kadhaa yanayotumia sarafu ya euro yamekumbwa na mgogoro wa kifedha na madeni, Strauss-Kahn alikuwa akichukuliwa kama rafiki na mshirika wa karibu, lakini sasa tayari kuna mawazo ya kufikiria kiongozi mpya wa IMF atakayeweza kufanya kazi na Umoja wa Ulaya.

Huyu hapa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye nchi yake imekuwa kinara wa mpango wa kuyanusuru mataifa ya Ulaya yanayotumbukia kwenye dimbwi la madeni kutokana na mgogoro wa kifedha:

"Naamini kwamba katika kipindi hiki tulicho sasa, ambapo tulikuwa tunajadiliana mengi kuhusiana na sarafu ya euro, kuna kila sababu kwa Ulaya kupata wagombea wazuri wa nafasi hii."

Kukamatwa kwa Strauss-Kahn kumekuwa pia aibu kwa taasisi yake ya IMF, kwani sasa maswali yamekuwa yakiulizwa juu ya namna taasisi hiyo ilivyomvumilia pale alipokutwa na kashfa ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mchumi wa Shirika hilo, ambaye pia alikuwa msaidizi wake hapo mwaka 2008.

Bodi ya IMF ilikutana hapo jana kwa kikao cha dharura kuhusiana na kesi hii, lakini msemaji wake, Caroline Atkinson, hakutoa ufafanuzi zaidi wa kikao hicho, zaidi ya kusema tu kwamba kilipokea taarifa ya mdomo kutoka kwa kaimu mkurugenzi mtendaji, John Lipsky, na mwanasheria wa shirika hilo, Sean Hagan. Uamuzi wa kumuachisha kazi Strauss-Kahn au la, bado haujatajwa. Kesi yake itatajwa tena hapo Mei 20.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters

Mhariri: Hamidou Oummilkheir