1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund, Bayern na Leverkusen zatamba Bundesliga

30 Septemba 2013

Timu zote zinazoshikilia uongozi wa msimamo wa ligi kuu ya soka hapa Ujerumani Bundesliga, Dortmund, Bayern na Leverkusen, zilisajili ushindi katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki

https://p.dw.com/p/19rku
Picha: picture-alliance/dpa

Borussia Dortmund waliwazidi nguvu Freiburg kwa kuwabamiza mabao matano kwa sifuri ijapokuwa walipoteza nafasi za wazi chungu nzima. Kwa sasa BVB wanaongoza ligi na pointi 19 kwa pamoja na Bayern Munich japo na faida ya magoli.

Vijana wa Pep Guardiola Bayern Munich nao walikuwa na sababu ya kumpongeza Thomas Müller aliyewafungia bao pekee katika ushindi wao waliotolewa kijasho na Wolsfburg. Leverkusen, wanasalia katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Bundesliga, baada ya kuwabwaga Hanover mabao mawili kwa moja. Sydney Sam ambaye ameoenekana kuijaza vyema nafasi iliyowachwa na Andre Schürrle aliyejiunga na Chelsea, msimu huu, alikuwa mmoja wa waliotikisa nyavu

Sydney Sam wa Leverkusen amelijaza vyema pengo lililowachwa na Andre Schurrle aliyehamia Chelsea
Sydney Sam wa Leverkusen amelijaza vyema pengo lililowachwa na Andre Schurrle aliyehamia ChelseaPicha: imago/Kolvenbach

Mambo hayawaendei vyema Schalke ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 14, baada ya kuduwazwa na sare ya mabao matatu kwa matatu na Hoffenheim licha ya kuwa walikuwa kifua mbele katika mchuano huo….katika mechi nyingine, Mainz waliendelea kudorora baada ya kuchabangwa mabao matatu kwa moja mbele ya mashabiki wao.

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi Bert van Marwijk alianza kibarua katika klabu yake mpya ya Hamburg kwa kutoka sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili na Enitracht Frankufurt. Van Marwijk aliwapongeza vijana wake baada ya mchuano uliowaweka katika nafasi ya 16.

Katika mechi zilizochezwa Jumapili, Werder Bremen walifungana mabao matatu kwa matatu na Nuremberg wakati nao Eintracht Braunschweig wakiendelea kushika mkia kwa kubamizwa mabao manne kwa sifuri na Stuttgart.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman