1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund kujiinua baada ya mwanzo mbaya

3 Oktoba 2014

Borussia Dortmund wanajiandaa kuwapiku Hamburg hii leo ili kumaliza msururu wa kutoshinda mechi tatu mfululizo katika Bundesliga, licha ya kuwa na kuanza vyema katika Champions League.

https://p.dw.com/p/1DPZo
Fußball 1. Bundesliga 6. Spieltag Schalke 04 - Borussia Dortmund 27.09.2014
Picha: Reuters/Ina Fassbender

Vijana wa Kocha Jurgen Klopp waliwabwaga Anderlecht mabao matatu kwa sifuri siku ya Jumatano, lakini matokeo ya kushindwa na Mainz na mahasimu wao Schalke, pamoja na sare waliyotoka na Stuttgart ya mabao mawili kwa mawili katika mechi zao tatu za mwisho, yamewaacha Dortmund na points saba pekee katika nafasi ya 12 ya msimamo wa ligi. Baada ya mechi sita pekee, BVB wako nyuma ya viongozi Bayern Munich na pengo la points sita. Sebastian Kehl ni kiungo wa BVB.

"Bila shaka pia tunafahamu kuwa hatujafanikiwa katika mechi chache zilizopita na tumefungwa magoli mengi. Na lengo letu kuu dhidi ya Anderlecht likuwa moja, kucheza vyema na kutofungwa goli. Tulikuwa imara na pia tukafanya mashambulizi makali. Lakini sasa lazima tufanye hivyo katika ligi ya nyumbani na tunauangazia mchuano dhidi ya Hamburg".

Fußball Bundesliga 5. Spieltag FC Bayern München SC Paderborn
Pe Guardiola ameshikilia usukani kileleni mwa BundesligaPicha: Reuters/Michael Dalder

Hamburg huwa wasumbufu sana kwa Borussia na wamewabwaga vijana hao wa Klipp mara tatu katika mechi nne na hivyo mchuano huo unatarajiwa kuwa mgumu. Kiungo mkongwe Sebastian Kehl huenda asicheze kutokana na jeraha dogo la mguu, lakini nahodha ambaye ni beki wa Ujerumani Mats Hummels anatarajiwa kurejea katika kikosi cha kwanza.

Hamburg ni mojawapo ya timu tatu pekee ambazo hazijasajili ushindi msimu huu na walishtushwa na habari mbaya siku ya Alhamisi wakati ilipithibitishwa kuwa kocha wa zamani Mirko Slomka aliwashtaki mahakamani kwa kumfuta kazi kinyume cha sheria mwezi jana baada ya mechi tatu pekee za msimu huu.

Hanover 96 wanasafiri ugenini Munich wakilenga kusajili ushindi wao wa kwanza nyumbani kwa Bayern tangu mwaka wa 2006, huku kocha wao Tayfun Korkut akiwapiga marufuku wachezaji wake kujumuika katika sherehe za kunywa pombe mjini Munich maarufu kama Oktoberfest ambazo zitakamilika kesho Jumapili.

Fußball 1. Bundesliga 5. Spieltag Bayer Leverkusen FC Augsburg
Bayer Leverskusen wanaonyesha kandanda safi chini ya kocha mpya Rodger SchmidtPicha: Reuters/Wolfgang Rattay

Hanover wako katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, lakini na pengo la points nne pekee nyuma ya viongozi Bayern kabla ya kivumbi chao katika ngome ya Allianz Arena. Nahodha wa Bayern Philipp Lahm anasema: "Tumepoteza points chache katika Bundesliga lakini hata hivyo tumepata ushindi mara mbili katika Champions League. Hivyo, tuko imara. Hilo lazima lisemwe wazi. Tunalenga tena kushinda wikendi. Tunaongoza msimamo wa ligi. Labda tunaweza kupanua pengo la uongozi kwa hivyo tuko katika hali nzuri. Hilo lazima lisemwe wazi".

Vijana wa mkufunzi Pep Guardiola wameangusha points nne pekee kufikia sasa msimu huu. Katika mechi nyingine za leo Juammosi, Bayer Leverkusen v Paderborn, Hoffenheim v Schalke 04, Werder Bremen v Freiburg, Eintracht Frankfurt v Cologne.

Kesho Jumapili timu ya Kocha Lucien Favre Borussia Moenchengladbach itaialika Mainz na timu zote mbili hazijashindwa mchuano wowote baada ya mechi zao sita msimu huu. VfL Wolfsburg v Augsburg.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu