1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaipiku Moenchengladbach

5 Desemba 2016

Borussia Dortmund iliigaragaza Borussia Mönchengladbach mabao 4-1 wakicheza nyumbani.

https://p.dw.com/p/2Tlp0
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund vs. Borussia Mönchengladbach
Picha: Getty Images/Bongarts/Ch. Koepsel

Borussia Dortmund iliigaragaza Borussia Mönchengladbach mabao manne kwa moja wakicheza nyumbani, huku mshambuliaji hatari wa Dortmund Pierre Emeric Aubameyang akifunga mabao mawili na kujipatia jumla ya mabao 15 na kuendelea kuongoza kama mfunganji bora katika Bundesliga. Ukionekana kama mtanange mkali kati ya mahasimu hao wa Borussia, mechi yenyewe ililalia upande mmoja huku Dortmund ikiutawala mchezo.

Mchezaji wa Monchengladbach, Christoph Krämer alisema, "Kidogo maji yamezidi unga, katika wiki zilizopita tulisema tungeshinda na leo tena tunasema tungelishinda. Lakini ukweli ni tofauti na kwa maana hiyo tuko katika kipindi kigumu na haisaidii kutilia shaka kila kitu. Hilo hatutakiwi kulifanya katika mazingira yoyote yale. Watu wameona jinsi tunavyowe kucheza kandanda. Sisi pia tunaweza kulinganishwa na Dortmund. Bao la tatu na nne kidogo tumeyasababisha wenyewe na kwa hiyo mambo yatakuwa magumu tutakapokwenda kucheza Dortmund."

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund vs. Borussia Mönchengladbach
Picha: Getty Images/Bongarts/Ch. Köpsel

Mechi nyingine ya kukata na shoka katika Bundesliga ilikuwa kati ya VfL Wolfburg na Hertha Berlin ambapo Hertha waliibuka kidedea magoli matatu kwa mawili katika uwanja wa Volkswagen Arena mjini Wolfsburg. Timu hizo zilikaribia kutoka sare mpaka pale mchezaji wa Hertha Plattenhardt alipofanyiwa madhambi ndani ya eneo hatari na kupewa penalti ambayo Salomon Kalou aliifunga na kuiwezesha Hertha kurejea nyumbani Berlin na pointi tatu.

Maximilian Arnold aliuleza hivi mchuano huo. "Katika kipindi cha pili tumeona kuwa Hertha wameshinikiza sana. Hatukuweza tena kufanya mashambulizi. Kisha wakakomboa ikawa mabao mawili kwa mawili, kitu ambacho tungetakiwa kukizuia kama sote tungerudi nyuma. Na katika dakika ya 90 ikatolea penalti. Hii inauma sana na inavunja moyo.

Leverkusen ilitoka sare ya bao moja kwa moja Freiburg nyumbani katika uwanja wao wa BayArena. Levekusen imefuzu kwa awamu ya mtoano katika mashindano ya kuwania ubingwa Ulaya, Champions League, lakini katika ligi ya nyumbani mambo hayawaendei vizuri. Leverkusen ilihangaishwa na Freiburg na kulazimika kutoka nyuma bao moja kwa bila kukomboa. Julian Brandt wa Leverkusen alisema, "Mtu anachukua kidogo kidogo na kujifunza. Mambo mengo hayaendi vizuri kwa sasa, na ni wazi bila shaka kwamba pia tulikosa penalti dakika ya 86. Hayo kwa ujumla ndiyo mambo yaliyotukabili katika wiki chache zilizopita."

Ushindi wa kwanza kwa Hamburg

HSV Hamburg ilionja ushindi kwa mara ya kwanza msimu huu ilipoizaba Darmstadt magoli mawili kwa bila katika mechi ya ugenini huko Darmstadt. Ushindi huo unaiondoa Hamburg katika nafasi ya 18 na kupanda hadi nafasi ya 17. Kocha wa Hamburg, Markus Gisdol alisema, "Haijabainika wazi kwangu kwamba tumefanya vibaya sana vile. Hatukufanya vyema katika michezo miwili iliyopita, tulikaribia kushinda angalau mechi moja. Leo tumestahiki ushindi huu na ulikuwa mwanzo mzuri."

Fußball Bundesliga SV Darmstadt 98 - Hamburger SV
Michael Gregoritsch wa Hamburg akifunga bao dhidi ya DarmstadtPicha: picture-alliance/dpa/R. Wittek

Hamburg, klabu pekee ambayo haijawahi kushuka daraja imekuwa ikivuta mkia tangu msimu huu ulipoanza mwezi Agosti.

Augsburg ilitoka sare ya bao moja kwa moja na Eintracht Frankfurt. Mchezaji wa Frankfurt Branimir Hrgota na Dong Won Ji wa Augsburg wote walizifungia timu na kujipatia bao la nane kila mmoja katika Bundesliga. Mshambuliaji machachari wa Frankfurt, Alexander Meier, alisema, "Leo tunaweza kuridhika. Tumecheza dakika 20 za kwanza vizuri sana, lakini baadaye tukapoteza kasi yetu. Nadhani kila upande umepata fursa sawa, kwa hiyo ni sawa na hatutakiwi kuvunjika moyo. Mechi kama hizi zipo, mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi. Tunashukuru kupata pointi moja."

Naye Daniel Baier wa FC Augsburg kwa upande wake alisema, "Kila tulichojaribu tena katika kipindi cha pili, kupiga mipira yote mbele, kukimbia; nadhani ulikuwa mchezo ambazo ungeshindwa na timu yoyote na kutoka sare ni haki. Ni wazi tungeweza kushinda, lakini mechi za ugenini zinakuwa ngumu. Kila wakati Frankfurt walikuwa hatari sana. Nadhani katika kipindi cha pili ulikuwa mchezo wenye sizani sawa na kwa hivyo sare ni haki kabisa."

Mwandishi:Josephat Charo/dpae/rtre/afpe

Mhariri:Yusuf Saumu