1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaivuka Hoffenheim katika nafasi ya tatu

Sekione Kitojo
8 Mei 2017

Pambano  lililojaa  hamasa  na  matarajio  kwa  pande  zote  kati  ya Borussia  Dortmund  na  TSG Hoffenheim  katika  Bundesliga lilimalizika  kwa  hisia  tofauti .Damstadt  yatoa  mkono  wa  kwaheri  kutoka  Bundesliga.

https://p.dw.com/p/2ccgy
1. Bundesliga 32. Spieltag |  Borussia Dortmund v Hoffenheim - Felix Brych
Refa Dr. Felix Brych akiashiria kwamba hataki kumsikiliza mchezaji wa Hoffenheim wakati akimlalamikiaPicha: picture alliance/AA/I. Fassbender

Katika  Bundesliga  katika  mchezo  wa  32 wiki  hii  kulikuwa  na msuguano  mkubwa  kati  ya  Borussia  Dortmund  na  TSG Hoffenheim  kuwania  nafasi  ya  tatu  inayohakikisha  timu itakayonyakua  nafasi  hiyo  kushiriki  katika  awamu  ya  makundi katika  Champions League  pamoja  na  tuzo  ya  euro  milioni  30. Uhakika  wa  kupata  tuzo  hiyo ndio uliufanya  mchezo  huo  kuwa muhimu  sana, ikitiliwa  maana  kwamba  timu itakayoteleza  kwenda nafasi  ya  nne itabidi  kuingia  katika  michezo  ya  mchujo  kabla  ya kuingia  katika  awamu  ya  makundi  ya  Champions League.

1. Bundesliga 32. Spieltag |  Borussia Dortmund v Hoffenheim - Felix Brych
Inaonesha ni namna gani pambano hilo lilivyokuwa na mvutano, mlinda mlango wa Dortmund Roman Bürki akimlalamikia refa Felix BrychPicha: Getty Images/S. Schuermann

Na  hii  Hoffenheim ilitaka  kuepuka  kwa  kuwa  ni  timu  isiyokuwa na uzoefu  katika  jukwaa  hili  la  kimataifa , na  huenda  ikakumbana na  baadhi  ya  vigogo  katika  bara  la  Ulaya  kama  kutoka  Itali, Uingereza  na  Uhispania  katika  kinyang'anyiro  hicho  cha  mchujo.

Borussia  Dortmund  ikicheza  nyumbani  iliibuka  kidedea  kwa ushindi  wa  mabao 2-1 dhidi  ya  Hoffenheim , lakini kwa  kweli kulitokea  makosa  mengi  yaliyofanywa  na  mwamuzi  wa  mchezo huo  Dr. Felix Brych  ambaye  ni  refa  bora  kabisa  nchini Ujerumani  na  hata  Ulaya  kwa  jumla. Alifanya  makosa  mara  mbili ambapo  aliruhusu  bao  la  kwanza  la  Borussia  Dortmund alilofunga  Marco  Reus akiwa  katika  nafasi  kabisa  ya  kuotea. Pili aliwapa  Dortmund mkwaju  wa  penalti  wakati  kabla  ya  hapo Marco  Reus  alionekana  kuutuliza  mpira  kwa  sehemu  ya  mkono wake  karibu  na  bega. Mkwaju  huo  wa  penalti  uliopigwa  na Pierre Emerick Aubameyang  hata  hivyo  uliishia  nje  ya  wavu. Huyu  hapa  Marco Reus  akizungumzia  matukio  hayo  katika mchezo  huo.

1. Bundesliga 32. Spieltag |  Bayern München - Darmstadt 98 - Fans
Wachezaji wa Hoffenheim wakijikusanya pamoja na kupeana hamasaPicha: picture alliance/dpa/M. Balk

"Sidhani  kama  refa  alitupendelea, kinyume  chake  kabisa. Lakini ni bila  shaka , ikiwa  niko mita  moja  katika  nafasi  ya  kuotea, ni lazima aamue haki, kwa  hiyo  ulikuwa  uamuzi  wa  makosa. Naamini , katika  msimu  huu  tumepata pia  kuadhibiwa kimakosa,  ambapo hatukuchukulia  kwamba  mwamuzi  ndio  aliyesababisha  hilo. Kwa hiyo  nadhani  kila  kitu kiko  sawa."

1. Bundesliga 32. Spieltag | Borussia Dortmund v TSG 1899 Hoffenheim
Wachezaji wa Dortmund wakishangiria bao katika mchezo huo dhidi ya HoffenheimPicha: Reuters/L Kuegeler

Hata  hivyo  kocha  wa  TSG  Hoffenheim  Julian  Nagelsmann hakuna  cha  kumtuliza  kutokana  na  makosa  yaliyotokea  katika mchezo  huo.

"Mshika  kibendera  alithibitisha  kwamba  goli  hio llikuwa  ni la kuotea. Lakini  amenithibitishia  kwamba , mwamuzi  ndio aliyeshikilia  kwamba  ni  goli  na  si  yeye. Pengine  hakuwa  na uwezo wa  kumshawishi  mwamuzi. Ninapoangalia  jinsi  mchezo ulivyokuwa  kati  ya  kikosi  changu  na  Dortmund ,  mchezo wetu ulikuwa  bora  zaidi, na  ndio  sababu ningetarajia  zaidi  ushindi."

Bado  kuna  michezo  miwili  kabla  ya  kumalizika  kwa  msimu  huu wa  Bundesliga , na  timu  hizo  zinakumbana  katika  michezo  hiyo miwili  na  timu mbili Werder  Bremen  na  Augsburg. Borussia Dortmund  inasafiri  kwenda  kupambana  na  Augsburg siku  ya Jumamosi ijayo, wakati TSG Hoffenheim nayo  inasafiri  kwenda kupambana  na  Werder  Bremen  nyumbani.

Deutschland Fußball Bundesliga Trainer Julian Nagelsmann
Kocha wa Hoffenheim Julian NagelsmannPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Mbali  ya  pambano  hilo  lililochukua  hisia  za  mashabiki  wa kandanda  nchini  Ujerumani , lakini  pia  klabu  ya  kandanda  ya  SV Damstadt  98 kwa  shingo  upande  ilibidi  kutoa  mkono  wa  kwaheri kwa  Bundesliga , baada  ya  kupokea  kipigo  cha  bao 1-0  kutoka kwa  mabingwa  wateule Bayern  Munich  licha  ya  wao  kukosa penealti  katika  dakika  ya  86  ambapo  mchezaji  wa  zamani  wa Bayern  Hamit  Altintop  alishindwa  kuuweka  mpira  wavuni  ambapo ulipanguliwa  na  mlinda  mlango  Tom Starke. Baada  ya  kudumu kwa  miaka  miwili  katika  Bundesliga  klabu  hiyo  inayotoka  katika jimbo  la  Hessen  kulazimika  kushuka  daraja.

1. Bundesliga 32. Spieltag |  Bayern München - Darmstadt 98 - Fans
SV Damstadt 98 yaaga Bundesliga na kuelekea daraja la pili msimu ujaoPicha: picture alliance/dpa/T. Hase

Hiyo  ni timu ya  kwanza  kushuka  daraja  msimu  huu, lakini mapambano  ya  kuwania  kubakia  katika  daraja  hilo  yanaendelea.

Wolfsburg  imepiga  hatua  kuelekea  kubakia  katika  daraja  la kwanza  kwa  kuikandika  Eintracht  Frankfurt  kwa  mabao  2-0 , na kuziacha  FSV Mainz  iliyoko  katika  nafasi  ya 15 na  SV Hamburg iliyoko  katika  nafasi  ya  16 kubakia  na  pointi  34 zikiwania  nafasi ya  16  ambayo inahusika  na  mchujo  wa  kubakia  katika  daraja  la kwanza. Timu  hizo zilitoshana  nguvu  jana  Jumapili  na  kumaliza mchezo  wao  bila  kufungana.

Kwa  upande  mwingine mbio za  kuwania  kucheza  katika  ligi  ya Ulaya , Europa League  zinaendelea , wakati  SC Freiburg imekoleza  moto  jana  baada  ya  kuishinda  Schalke  04   kwa mabao 2-0  , hali  inayoikatisha  tamaa  Schalke  kucheza  Ulaya msimu ujao. Mchezaji  wa kati  wa  Schalke  04 Leon Goretzka alikuwa  na  haya  ya  kusema.

Bundesliga SC Freiburg vs FC Schalke 04 - Bundesliga
Kinyang'anyiro kati ya Marc-Oliver Kempf wa Freiburg akipambana na Daniel Caligiuri wa SchalkePicha: Getty Images/Bongarts/S. Hofmann

"Baada  ya  kufungwa  bao la  pili  katika  kipindi cha  kwanza Freiburg  ilijiweka  katika  nafasi  nzuri  sana. walitufanya  tushindwe kabisa  kucheza  mchezo  wetu, licha  ya  kuwa  walicheza  nyumbani na  hii  kwa  kweli  imetuathiri  sana  msimu  huu."

Hertha BSC  Berlin  ilipokea  kipigo  cha  mabao 4-1 siku  ya Jumamosi  na  matumaini  yao  ya  kucheza  kombe  la  ligi  ya Ulaya  pia  yanalegalega , kama  ilivyo  kwa  FC Kolon  ambayo licha  ya  kuishinda  Werder  Bremen  kwa  mabao 4-3  siku  ya Ijumaa  sasa  imefikisha  pointi  moja  nyuma  ya  Hertha  Berlin kuweza  kufikia  nafasi  hiyo ya  kucheza   kombe  la  ligi  ya  Ulaya.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Josephat Charo